SERIKALI YA AWAMU YA SITA YALETA MAPINDUZI YA MAENDELEO SHINYANGA KWA VITENDO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 4 May 2025

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YALETA MAPINDUZI YA MAENDELEO SHINYANGA KWA VITENDO



NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL SHINYANGA

Katika kuendeleza dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi. Safari hii, moto huo wa maendeleo umewashwa mkoani Shinyanga, ambako miradi ya kilimo, elimu, na miundombinu imepewa kipaumbele kikubwa kwa lengo la kuibadilisha taswira ya mkoa huo.


Akizungumza Mei 3, 2025 katika kijiji cha Sayu, Kata ya Pandagichiza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, ameeleza hatua madhubuti zinazochukuliwa na Serikali ili kuimarisha kilimo cha kisasa hususani katika zao la pamba.


Katika juhudi hizo, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 17 kwa ajili ya kukuza kilimo hicho, ikiwa ni pamoja na kuleta vifaa vya kisasa na kuwajengea uwezo Maafisa Ugani kwa mafunzo na vifaa vya kazi Ikiwemo kuwapatia pikipiki kwa ajili ya kuwarahisishia usafiri maafisa hao.


Msigwa amewataka wakulima wa pamba mkoani Shinyanga kubadili mtazamo na kutumia mbinu za kitaalamu za kilimo ili kuongeza uzalishaji ambapo ameeleza kuwa kwa msimu uliopita mavuno yalikuwa kilo milioni 22, sawa na kilo 300 kwa hekari, kiwango ambacho ni kidogo.

Msigwa ameeleza kuwa Serikali inaamini kupitia mbinu mpya na teknolojia, uzalishaji unaweza kufikia kilo milioni 300 msimu huu, jambo litakaloongeza thamani ya zao hilo na kuwaongezea tija wakulima.


Katika sekta ya elimu, Msigwa alitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga na kueleza kuwa Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 4 kujenga miundombinu ya kisasa ya shule hiyo. Lengo ni kutoa mazingira bora kwa wanafunzi wa kike na walimu, na kuhakikisha shule hiyo inakuwa miongoni mwa shule bora kabisa nchini. Shule hiyo maalum ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike, ikiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita katika mchepuo wa Sayansi.


Akizungumzia maendeleo ya miundombinu, Msigwa ametembelea pia uwanja wa ndege wa Shinyanga unaojengwa katika Kata ya Ibadakuli ambapo Uwanja huo umefikia asilimia 80 ya ujenzi, unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2025 kwa gharama ya shilingi bilioni 44.8, Mradi huu ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya Serikali katika kuimarisha usafiri wa anga na kuchochea uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.


Ziara ya Msemaji Mkuu wa Serikali mkoani Shinyanga imetoa taswira kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na dhamira ya dhati ya Rais Samia kuwaletea Watanzania maisha bora, Miradi hii inaweka msingi imara wa maendeleo ya muda mrefu katika kilimo, elimu, na miundombinu Mkoani Shinyanga.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso