Na Neema Nkumbi - Kahama, Mei 29, 2025
Katika hatua ya kuendeleza juhudi za serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo, hususan wanawake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, ameahidi kuwapatia wanawake wa Chama cha Wanawake Wachimbaji wa Madini Tanzania (TAWOMA) makarasha 10 ili kuwawezesha katika shughuli zao za uchimbaji na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwenye semina ya mafunzo kwa wanawake wachimbaji wa madini iliyofanyika leo mjini Kahama, Dkt. Mwasse amesema, “Njia sahihi ya kuhakikisha wananchi wanavuna rasilimali ni pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogo au wazawa ili waweze kuchimba kwa tija”, hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuhakikisha ushiriki wa wananchi katika sekta ya madini unakuwa wa tija na unaochochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwasse, TAWOMA ina mchango mkubwa katika ajira kwa wanawake ambapo kati ya ajira milioni sita zinazotokana na wachimbaji wadogo, wanawake wanashikilia zaidi ya milioni tatu sawa na asilimia 52.
Naye Mwenyekiti wa TAWOMA Taifa, Bi. Semeni Malale, ameeleza kuwa chama hicho kimeweza kuchangia zaidi ya shilingi bilioni nne katika mapato ya serikali pia amesisitiza umuhimu wa wanawake kuaminiwa na kupewa vifaa vya kisasa vya kutafiti miamba ya madini ili kuimarisha uwekezaji wao na kuepuka kutegemea imani potofu.
“Mabenki pia yawaamini akinamama kwa kuwapa mikopo na leseni za uchimbaji ili waweze kufanya shughuli zao kwa kujiamini,” amesema Semeni.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Bw. Hamza Tandiko, ameiomba TAWOMA kutanua wigo wake kwa kuwajumuisha wanawake wanaochimba madini mengine kama almasi na kupendekeza kuwepo kwa mafunzo endelevu yatakayowawezesha wachimbaji hao kufuata sheria na taratibu za uchimbaji salama na endelevu.
Miongoni mwa wachimbaji wanawake waliopata fursa ya kuhudhuria semina hiyo, Bi. Agnes Kahabi ameeleza kuwa kutokana na uhaba wa ajira, vijana wengi wasomi na wasio wasomi wamekimbilia kwenye sekta ya madini.
Agnes amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa wa namna ya kujilinda kiafya, kutunza fedha na hatimaye kuinuka kiuchumi.
No comments:
Post a Comment