Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa rai nzito kwa viongozi wa chama hicho kuhakikisha mchujo wa wagombea unaendeshwa kwa haki na kwa kuzingatia maslahi mapana ya chama na taifa.
Akihutubia wakati wa kufunga Mkutano Maalum wa CCM uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma, Mei 30 2025 –Dkt. Samia amesisitiza kuwa vikao vya uteuzi visifanyike kwa upendeleo wala kushinikizwa na matakwa ya watu binafsi, bali vizingatie sifa, uwezo na maadili ya wagombea.
“Vikao vinavyokwenda kuchuja watu, vinavyokwenda kuchuja wagombea, wakatende haki. Anayefaa aambiwe anafaa, asiyefaa tuseme huyu ana kasoro moja mbili tatu, hatufai huko mbele tunapokwenda,” amesema Dkt. Samia kwa msisitizo.
Aidha, ameonya dhidi ya tabia ya kupitisha wagombea kwa misingi ya ushawishi wa muda mfupi au makundi ya maslahi binafsi, akisema:
“Tukitoa mwanya na kupitisha wanaotafuta tu, na mie niwemo, ndiyo tunapata wale waokwenda huko, Chama kinakuwa Gwajimanised. Kwa namna yoyote, tusigwajimanise Chama chetu, magwajima tuyaache nje. Hakuna kuoneana aibu wala haya.”
Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa kuwapima wagombea kwa sifa, maadili na uwezo wao, siyo kwa mapenzi binafsi, hofu au mahusiano ya karibu huku akionya kuwa mtu ambaye hana uhusiano wa kweli na chama hawezi kusaidia, bali atakivuruga.
"Mcheza ngoma si yake lazima ataharibu, ukicheza ngoma si yako utaharibu na utajulikana tu",ameongeza Dkt. Samia.
No comments:
Post a Comment