Mkurugenzi wa shirika la Women and Youth Development Solution (WAYDS) Charles Deogratius, akiwa katika kongamano la afya ya akili
NA NEEMA NKUMBI- KAHAMA
Vijana wa Tanzania wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za afya ya akili kimya kimya wakihangaika na msongo wa mawazo, uraibu wa dawa za kulevya na matatizo ya familia bila msaada wa kutosha, hali iliyoibua mjadala mpana kitaifa baada ya kufanyika Mkutano wa Kitaifa wa Afya ya Akili kwa mara ya kwanza katika mkoa wa Shinyanga, lengo kuu likiwa ni kuweka vijana mstari wa mbele katika harakati za kutatua tatizo hilo.
Mkutano huo umeanza rasmi leo katika Manispaa ya Kahama, ukiandaliwa na shirika la Women and Youth Development Solution (WAYDS), ambapo Mkurugenzi wa WAYDS, Charles Deogratius, ameeleza kuwa ni wakati wa taifa kuwekeza kwa dhati katika afya ya akili, hasa kwa vijana, kwani hakuna maendeleo bila ustawi wa akili.
“Afya ya akili ni msingi wa maendeleo, lakini hatuwezi kufikia maendeleo hayo bila kufanya kazi kwa pamoja, kuweka sera bora na kuwa na takwimu sahihi kuhusu waathirika,” amesema Deogratius.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akimwakilisha Waziri wa Afya Jenista Mhagama, amesema serikali tayari imeanza kuchukua hatua madhubuti kwa kutenga TSh milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa kituo maalum cha kusaidia waraibu wa dawa za kulevya, ambao ni sehemu kubwa ya waathirika wa matatizo ya akili.
Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watu Wenye Ulemavu Tulo Masanja, ameeleza kuwa majanga kama mafuriko, ajali au migogoro ya familia huzua mshtuko wa kisaikolojia unaoathiri afya ya akili, hivyo kuna umuhimu wa kutoa huduma za msaada haraka na kwa mujibu wa sheria za taifa.
“Tunaandaa miongozo ya kitaifa ya huduma za afya ya akili wakati wa majanga, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kuhakikisha kila mtu anapata msaada wa haraka,” amesema Tulo.
Afisa Habari wa Hospitali ya Mirembe, Christian Elias, amebainisha kuwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 35 ndio wanaoathirika zaidi, kutokana na presha ya maisha na matumizi ya dawa za kulevya.
Rehema Hussein, kijana aliyenusurika na ugonjwa wa akili uliosababishwa na manyanyaso ya ndoa amesimulia namna alivyojaribu kutafuta msaada baada ya kufikiria kujiua pamoja na mtoto wake wa miezi minne kutokana na msongo wa mawazo.
“Nilifika hatua ya kutaka kujiua mimi na mwanangu, lakini nilipata msaada kutoka dawati la jinsia polisi na baadaye vikundi vya vijana na mazoezi vilinisaidia kujitambua na kupona,” amesema Rehema.
No comments:
Post a Comment