NA NEEMA NKUMBI -HUHESO DIGITAL KAHAMA
Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mtaa na Vijiji katika Kata ya Mhongolo, zilizoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimehitimishwa rasmi leo, Novemba 25, 2024, kwa mkutano mkubwa uliofanyika katika kijiji cha Mhongolo.
Mkutano huo umeongozwa na viongozi wa CCM kutoka Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya Kahama, ambapo wamesisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi watakaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi.
Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Shinyanga, Benard Wilson, ametoa wito kwa viongozi watakaochaguliwa kuwasikiliza wananchi na kuacha kutangaza changamoto zao badala ya kuzitatua.
“Chama cha Mapinduzi tunahitaji viongozi wanaoenda kusikiliza wananchi”, Amesema Benard.
Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila, amesisitiza kuwa CCM ina historia ya kuleta maendeleo na kwamba kimeandaa muongozo wa kutekeleza majukumu ya viongozi, hususani katika maeneo ya miundombinu, elimu, na afya.
"Muongozo huu utawasaidia viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao", amesema Simbila.
Mgombea Uwenyekiti Mtaa wa Mhongolo, Emanuel Nangale, ameelezea dhamira yake ya kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi, elimu, afya, na miundombinu katika mtaa wake huku akisisitiza kwamba kipaumbele chake ni kuanzisha shule ya sekondari hadi kidato cha sita katika Mhongolo.
Kampeni hizo zimemalizika kwa salamu za matumaini na wito wa amani, huku viongozi wakihimiza wananchi kuendelea kuwa na imani na CCM kama chama kinachoweza kuleta mabadiliko chanya katika taifa zima.






















No comments:
Post a Comment