TFF WAMSIMAMISHA KAZI KOCHA MKUU WA TAIFA STAR - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 19 January 2024

TFF WAMSIMAMISHA KAZI KOCHA MKUU WA TAIFA STAR

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemsimamisha kazi Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mualgeria Adel Amrouche na kumteua mzalendo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuwa Kaimu Kocha Mkuu.



Hatua ya TFF inafuatia Shirikisho la Soka Afrika kumfungia mechi nane Amrouche baada ya kutoa kauli zisizo za kiungwana dhidi ya Morocco kuelekea mchezo wa kwanza wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Jumatano wiki hii.


Amrouche aliituhumu Morocco kuwa inajipangia muda wa kucheza mechi zake na marefa wa kuchezesha pia akilenga kuaminisha ni kwa sababu hiyo wanafanya vizuri.


Simba wa Atlasi, Morocco wailifunga Tanzania, Taifa Stars 3-0 kwenye mchezo huo wa ufunguzi wa Kundi F Jumatano Uwanja wa Laurent Pokou Jijini San-Pedro nchini Ivory Coast.
Mabao ya Simba wa Atlasi yalifungwa na beki wa Al-Shabab ya Saudí Arabia, Romain Ghanem Paul Saïss dakika ya 30, kiungo wa Marseille ya Ufaransa, Azzedine Ounahi na mshambuliaji wa Sevilla ya Hispania, Youssef En-Nesyri dakika ya 80.


Taifa Stars ilimaliza pungufu baada ya kiungo wa Shakhtar Donetsk ya Ukraine Novatus Dismas Miroshi kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 70 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.


Taifa Stars inatarajiwa kuteremka tena Uwanja wa Uwanja wa Laurent Pokou Jijini San-Pedro Jumapili Saa 2:00 usiku kumenyana na Zambia katika mchezo wa pili wa Kundi F, siku ambayo Morocco itamenyana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Saa 11:00 Jioni hapo hapo Uwanja wa Laurent Pokou.


Morocco inaongoza Kundi F kwa pointi zake tatu, ikifuatiwa na DRC na Zambia zenye pointi moja kila moja, wakati Tanzania inashika mkia ikiwa haina pointi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso