WANANCHI WASHAURIWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA ZAO KABLA YA KUINGIA KWENYE NDOA, KUEPUKA KUZAA WATOTO WENYE UGONJWA WA SELI MUNDU - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 29 September 2023

WANANCHI WASHAURIWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA ZAO KABLA YA KUINGIA KWENYE NDOA, KUEPUKA KUZAA WATOTO WENYE UGONJWA WA SELI MUNDU


UGONJWA wa selimundu (Sickle Cell Desease) kwa watoto wachanga, unaweza kupunguzwa au kukatwa mnyororo wa thamani endapo wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa watapima afya zao kujitambua hali zao.


Dkt. Sophia Mosha akiendelea na uelimishaji kuhusu ugonjwa wa Selimundu katika shule ya sekondari ya Ihungo iliyoko Manispaa ya Bukoba.


NA MUTAYOBA ARBOGAST, HUHESO DIGITAL-BUKOBA


Hii inatokana na kuwa ugonjwa huo wa selimundu ni ugonjwa wa kurithi, ambao unarithiwa kutoka kwa baba na mama wote wawili na sio kwa mzazi mmoja tu, hivyo kupima afya kabla ya kuingia kwenye ndoa ni suala muhimu kwani husaidia wanaopanga kufunga ndoa kujijua kama wana vinasaba vya selimundu wote kwa pamoja au hawana


Nasaha hizo zimetolewa na wataalamu wa Afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba (BRRH) walipotembelea shule za sekondari Rugambwa, Kaizilege, na Ihungo zilizoko manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na kutoa elimu kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ikiwa ni mwendelezo wa utoaji elimu kwa jamii juu ya ugonjwa wa selimundu.


"Tunapowashauri wananchi kupima kabla ya kuanzisha familia lengo ni wasiende kuwa na wenza ambao wote (mme na mke) wana vinasaba vya ugonjwa wa selimundu, mkipima mapema na kuhakikisha hamna vinasaba au mmoja anavyo mwingine hana mnapata uhakika wa mtoto atakayepatikana atakuwa hana ugonjwa huo, hapa tutakuwa tumekata mnyororo”, amesema Dk Sophia Mosha wakati wa uelimishaji, ambapo mwezi Septemba kila mwaka huwa ni wiki ya uelimishaji kuhusu ugonjwa wa selimundu ikiwa ni njia moja wapo ya kupambana na ugonjwa huo.


Dk Sophia ameongeza kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba mwezi huu , wanatoa huduma ya upimaji wa awali kwa watoto wote wanaozaliwa katika hospitali hiyo na ikibainika mtoto ana ugonjwa huo anaanzishiwa klini na atafuatiliwa ili aweze kusaidiwa kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa na Wizara ya Afya na baada ya mwezi huu huduma ya upimaji kwa lika zote itaendelea kutolewa kama kawaida kwa kuchangia kiasi kidogo lengo likiwa ni kupambana na ugonjwa huu.


Naye Dk. Immaculate Kalungi amesema kuwa, dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mtu kuishiwa damu mara kwa mara, kuwa na macho ya njano, kuvimba paji la uso, kuugua mara kwa mara pamoja na ukuaji hafifu kwa upande mtoto.

Dk.Immacute Kalungi pamoja na wataalamu wengine wa Afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Bukoba (BRRH) wakiendelea na uelimisha juu ya ugonjwa wa Selimundu katika shule ya sekondari Rugambwa iliyoko Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.


Kwa upande wake, Privatus Selestine ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita (PCM) shule ya sekondari Ihungo , amewapongeza wataalamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba kwa kuwatembelea na kuwapatia elimu juu ya ugonjwa huo, huku akisema kuwa wao kama vijana watakuwa mabalozi kwa jamii zao ili waone umuhimu wa kupima afya kabla ya kuingia kwenye ndoa huku akisisitiza kuwa nao watazingatia ushauri huo pindi watakapo fikia utu uzima na kutaka kuingia kwenye ndoa.


Hospitali ya Rufaa Mkoa, Bukoba kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wanaungana na Dunia nzima kuadhimisha mwezi huu kwa kutoa elimu, ushauri na upimaji wa awali wa ugonjwa wa selimundu kwa watoto pamoja na watu wazima.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso