BREAKING NEWS: MKURUGENZI WILAYA YA MVOMERO ASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday 20 April 2022

BREAKING NEWS: MKURUGENZI WILAYA YA MVOMERO ASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Hassani Njama ili kupisha uchunguzi.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais –TAMISEMI Nteghenjwa Hosseah, imeeleza kuwa Waziri Bashungwa amechukua hatua hiyo leo Jumatano April 20, 2022 baada ya Mkurugenzi huyo kushindwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya Machi 10,2022 Wilayani humo.

Taarifa imeeleza kuwa Wakati wa ziara hiyo Waziri Bashungwa alibaini upotevu wa Fedha za miradi na matumizi yasiyo sahihi ya kiasi cha shilingi milioni 231.84 katika ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Moringe Sokoine.


Fedha hizo zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula, jiko na bweni na kumuagiza Mkurugenzi huyo kuwachukulia hatua za kiutumishi Wakuu wote wa Idara na watumishi waliohusika na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi katika mradi huo.

Taarifa imeeleza kuwa hadi kufikia leo hakuna Mkuu wa Idara yeyote ama mtumishi aliyechukuliwa hatua kufuatia maagizo hayo.

Aidha Waziri Bashungwa ameendelea kuwataka Wakurugenzi wa Halmashuri zote nchini kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo kikamilifu na kuchukua hatua za haraka pale wanapobaini ubadhifu wa fedha za umma.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso