Ajali iliyohusisha lori la mafuta na lori lililobeba saruji katika kijiji cha Isaka, kata ya Isaka wilayani Kahama mkoani Shinyanga, na kusababisha uharibifu wa magari na majeruhi.

Mkuu wa kituo cha zimamoto na uokoaji wilaya ya Kahama Hafidhi Omari, akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Isaka, kata ya Isaka, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga kuhusu madhara ya kuchota mafuta pindi magari ya kubeba mafuta yanapopata ajali kwenye maeneo yao.


Na Mwandishi wetu - Kahama


Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, limefanikiwa kuzuia hatari ya mlipuko wa moto baada ya lori la mafuta kuligonga kwa nyuma lori la lililokuwa limebeba saruji katika Kata ya Isaka, Halmashauri ya Msalala.


Tukio hilo limetokea Aprili 8, 2026, na linadhihirisha weledi na ujasiri wa askari hao katika maokozi na kudhibiti ajali zenye hatari kubwa kwa maisha ya binadamu na mali.


Lori la mafuta lenye namba T 668 EPA (kichwa) na T 210 CWM (tela), mali ya kampuni ya Ngara Huduma, lilikuwa likisafirisha petroli kutoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Kagera.


Kwa upande mwingine, lori la saruji lenye namba RAI 819V (kichwa) na RL 7622 (tela), mali ya kampuni ya FRESAR, lilikuwa likitokea Tanga kuelekea Rwanda likiendeshwa na Dufitumukiza Anselme (38), raia wa Rwanda.


Mkuu wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Kahama, Hafidhi Omari, amesema walipokea taarifa ya tukio hilo kupitia namba ya dharura ya zimamoto 114, ambapo baada ya kikosi chake kufika eneo la tukio, walichukua hatua za haraka za kudhibiti hatari ya mlipuko kutokea.


Amesema kwa kushirikiana na vyombo vingine, usalama wa eneo hilo uliimarishwa huku shughuli ya kubadilisha kichwa cha lori la mafuta ikikamilika salama kutokana na kuharibika vibaya.


Amesema magari yote mawili yaliokolewa, na zoezi la ubadilishaji wa kichwa kwenye lori la mafuta limekamilika salama huku lita zaidi ya 34,000 za petroli zikiokolewa bila kusababisha mlipuko wala madhara zaidi kwa binadamu.


“Tulishauri njia salama ni kubadilisha kichwa cha lori kuliko kuhamisha mafuta kwenye lori lingine hatua inayoweza kusababisha kutokea mlipuko kirahisi endapo mafuta ambayo ni kimiminika kiwakacho kitakutana na hali ya joto linaloweza kusababishwa na msuguano wa vyuma kwenye gari, joto la kwenye engine, cheche za short ya umeme au kwenye battery au uwashaji wa sigara.” Amesema Omari na kuongeza


“ Tumebadili kichwa cha lori la mafuta na kuhakikisha eneo lote linakuwa salama kwa kufanya fire cover ya njia mbili za kutupa maji malumu ya kuzimia yaliyochanganyika na povu (Foam compound).”




Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi.


Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori la mafuta, ambaye aliendesha bila tahadhari na hivyo kuligonga kwa nyuma lori la saruji lililokuwa limeegeshwa pembeni wakati dereva wake akisubiri kugonga mhuri kwenye nyaraka ofisi za TRA, Isaka.


Amesema kutokana na ajali hiyo zaidi ya lita 7,000 za petrol zilimwagika, lakini juhudi kubwa za jeshi hilo kwa kushirikiana na zimamoto, walifanikiwa kudhibiti uhalifu pamoja na mlipuko wowote katika eneo hilo.


"Zaidi ya lita 7,000 za petrol zimemwagika, lakini nalipongeza sana jeshi la zimamoto Kahama na Shinyanga kwa ujumla wake kwani juhudi ni kubwa zilifanyika kudhibiti mlipuko kwenye eneo lile pamoja na uhalifu." Amesema Magomi na kuongeza


"Kwa kweli Zimamoto wamejitahidi sana, na hii ni kwa sababu magari tunayo ya kutosha na vyombo vyetu vipo imara wakati wote kukabiliana na majanga yoyote yanapojitokeza."


Amesema ajali hiyo ilisababisha majeruhi kwa mtu mmoja Gidion Ibrahimu (24), mkazi wa Katoro mkoani Geita, ambaye alikuwa abiria kwenye lori la mafuta na anaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Isaka.


Amewaasa madereva kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani, na kwamba jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka sheria hizo.


Hatua hiyo pia imeondoa taharuki kwa wakazi wa eneo hilo, ambao walitoa pongezi zao kwa askari wa zimamoto kwa ujasiri, weledi na juhudi zao za dhati kudhibiti tukio hilo bila kusababisha mlipuko.


ELIMU




Kufuatia ajali hiyo, jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, kupitia kitengo cha mawasiliano na uhusiano kwa umma, limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kinga na tahadhari za majanga ya moto, hususan hatari ya kuchota mafuta kutoka kwenye magari yanayopata ajali.


Elimu hiyo imetolewa kwa wananchi wa Kijiji cha Isaka, kata ya Isaka, Halmashauri ya Msalala, ikiwa ni sehemu ya juhudi za jeshi hilo kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu usalama na namna ya kuepuka madhara yanayoweza kuzuilika.


Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Mkuu wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Kahama Hafidhi Omari, amewapongeza wananchi wa Isaka kwa kuwa watulivu na kujiepusha kuchota mafuta pale lori la mafuta lilipopata ajali kwenye kijiji hicho.


Amesema kitendo cha wananchi kukimbilia kuchota mafuta inapotokea ajali ni hatari na kinaweza kusababisha mlipuko na moto unaoweza kusababisha madhara kwa binadamu na mali.


Omari amewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa wakati pale wanapoona dalili za moto au tukio la ajali kwa kupiga namba ya dharura 114, ili kuwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika kwa haraka na kuchukua hatua stahiki.


Amesema “Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuzingatia maelekezo ya usalama yanayotolewa mara kwa mara, ili kujilinda dhidi ya majanga ya moto na kuchangia katika kuimarisha usalama wa jamii kwa ujumla.”

Muonekano wa mbele wa lori la mafuta baada ya kupata ajali katika kijiji cha Isaka, kata ya Isaka wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, wakiendelea na shughuli ya udhibiti wa mlipuko wa moto baada ya lori la mafuta kugongana na lori la lililokuwa limebeba saruji, katika kijiji cha Isaka, kata ya Isaka, Halmashauri ya Msalala. pembeni ni baadhi ya mifuko ya saruji.


Muonekano wa lori la mafuta baada ya kubadilishwa kichwa kilichoharibika vibaya baada ya kugongana na lori la saruji katika kijiji cha Isaka, kata ya Isaka, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.


Katika picha elimu ikiendelea kutolewa kwa wananchi wa kijiji cha Isaka, kata ya Isaka, Halmashauri ya Msalala kuhusu athari za kukimbilia kuchota mafuta wakati malori yanapopata ajali.👇👇