Mkuu wa Mkoa wa shinyanga Mboni Mhita akizungumza na wananchi mara baada ya kusikiliza kero mbali mbali za wananchi wa Manispaa ya Kahama.
Na Neema Nkumbi, Kahama
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wameiomba Serikali kuangalia upya masharti ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, wakieleza kuwa vigezo vilivyopo vinawakatisha tamaa walengwa na kuwasukuma kukimbilia mikopo isiyo rasmi maarufu kama kausha damu.
Mikopo hiyo inasimamiwa na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kifungu cha 37A, kinachozielekeza Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake (asilimia 4), vijana (asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2).
Malalamiko hayo yametolewa Januari 14, 2026 katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Daniel Ikango, mkazi wa Nyakato, alisema licha ya kufuata taratibu zote ikiwemo kuunda vikundi, kuandaa katiba na kufungua akaunti za benki, bado wanakumbwa na masharti yanayowavunja moyo.
“Tulielekezwa kuunda vikundi vya wajasiriamali wadogo, tukafanya kila tulichoelekezwa, lakini mwisho tunaambiwa sharti uwe mmiliki wa nyumba ili upate mkopo. Nauliza, hizi pesa ni kwa watu wa kipato gani hasa?” amehoji Ikango.
Kwa upande wake, Sofia Mbacha, mkazi wa Nyasubi, amesema wanawake wameitikia wito wa Serikali wa kujishughulisha na shughuli za kiuchumi, lakini mchakato mrefu na masharti magumu ya mikopo hiyo umewafanya wengi kukata tamaa.
“Akina mama tumeshaamka kufanya kazi kusaidiana na familia zetu, lakini hii mikopo tangu mwaka juzi imekuwa na mzunguko mrefu sana. Unarudishwa mara kwa mara mpaka unakata tamaa, ndipo tunaingia mikopo ya kausha damu na familia zinaanza kuyumba,” amesema Sofia.
Naye Stanslaus Rumbika, akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu, ameiomba Serikali kurejesha na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya ujasiriamali kwa kundi hilo, akisema ni miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, amesema mikopo hiyo imekuwa ikitolewa kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizopo, huku akitoa takwimu za fedha zilizokwisha tolewa kwa walengwa.
Kibetu amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri imetoa zaidi ya Shilingi milioni 714.6 kwa vikundi vya vijana, wanawake walipatiwa zaidi ya Shilingi milioni 738, huku watu wenye ulemavu wakipata zaidi ya Shilingi milioni 35.
Ameongeza kuwa katika awamu ya pili iliyoishia Desemba 2025, jumla ya zaidi ya Shilingi milioni 873.8 zilitolewa, ambapo wanawake walipata zaidi ya Shilingi milioni 448 na vijana zaidi ya Shilingi milioni 426.
Amesema kutokana na uwepo wa vikundi vingi vyenye mahitaji, Manispaa imejipanga kuvifikia vikundi vyote vinavyokumbwa na changamoto na kutoa elimu ili viweze kunufaika na mikopo hiyo.
“Ni kweli vikundi bado ni vingi na changamoto wanazozizungumzia huenda zipo, lakini sisi kama Manispaa ya Kahama tutavifikia na kuwapa elimu. Fedha zipo, lengo ni kuhakikisha zinawanufaisha walengwa waliokusudiwa,” alisema Kibetu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameielekeza Halmashauri hiyo kuwasimamia kwa karibu wataalamu wa maendeleo ya jamii ngazi ya kata ili kuhakikisha vikundi vinapata ushauri sahihi tangu hatua za awali, hivyo kuondoa usumbufu unaojitokeza nyaraka zinapofika ngazi ya wilaya.
“Haiwezekani nyaraka zipitie kata bila shida, halafu zikifika Halmashauri zikaambiwa hazikidhi vigezo. Afisa maendeleo ngazi ya kata anapaswa kuwashauri ipasavyo kwa kuwa ndiye anayepokea maelekezo ya juu,” amesisitiza Mhita.
Itakumbukwa kuwa Aprili 2023 Serikali ilisimamisha kwa muda utoaji wa mikopo ya asilimia 10 baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini mapungufu makubwa katika usimamizi wa mikopo hiyo kwenye mamlaka za serikali za mitaa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapungufu yaliyobainishwa ni pamoja na Halmashauri kushindwa kutenga fedha hizo, marejesho duni ya mikopo, utoaji wa mikopo kwa vikundi visivyofanya biashara, vikundi hewa, pamoja na kutoa mikopo kwa watu wenye ajira rasmi kinyume na taratibu.
Ripoti hiyo pia ilieleza kushindwa kutenga fedha za usimamizi na ufuatiliaji wa mikopo, pamoja na kutohusishwa kwa wataalamu wa usimamizi wa mikopo, hali iliyosababisha kuongezeka kwa mikopo chechefu.
Mwisho.










No comments:
Post a Comment