Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji imetoa wito kwa wawekezaji wote nchini, hususan wawekezaji binafsi, kujisajili katika taasisi ya TISEZA ili iwe rahisi kuwatambua, kutatua changamoto zao na kuwashirikisha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini.
Wito huo umetolewa Januari 10,2026 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Kahama mkoani Shinyanga, ambapo ametembelea Kongani ya Buzwagi pamoja na kiwanda cha Musumba Steel Tanzania Limited kinachozalisha bidhaa mbalimbali za ujenzi ikiwemo mabati, misumari, mabomba na bidhaa nyingine za chuma.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Chaya amesema Serikali ina wajibu wa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili waweze kuwekeza na kufanya shughuli zao kwa ufanisi ameongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara yake kuwahudumia na kuwalea wawekezaji waliopo kupitia taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Maeneo ya Viwanda Tanzania (TISEZA) ambayo ina ofisi ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwahudumia wawekezaji kwa karibu.
“Mwaka 2025 Mheshimiwa Rais alitengeneza Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ambayo ni dira ya 2050, ambapo kipaumbele kikubwa ni uwekezaji wa ndani na nje ya nchi ndiyo maana tunahamasisha wawekezaji kujisajili TISEZA ili waweze kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo,” amesema Dkt. Chaya.
Ameeleza kuwa Tanzania imefungua milango kwa wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali, akimtaja mwekezaji wa Musumba Steel ambaye ni mwekezaji kutoka Burundi kuwa mfano mzuri wa uwekezaji wa kigeni unaochangia maendeleo ya taifa na kusema kwamba Serikali imepokea changamoto za mwekezaji huyo na itaendelea kushirikiana na wizara na taasisi husika kuhakikisha uwekezaji huo unaendelea kukua katika mazingira ya amani, usalama na utulivu.
Dkt. Chaya ameongeza kuwa wilaya ya Kahama ina maeneo makubwa yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji ikiwemo Kongani ya Buzwagi, huku miundombinu muhimu kama umeme, maji, barabara na uwanja wa ndege kuwa vinapatikana hivyo amewaomba wawekezaji waliopo kuwa mabalozi kwa wawekezaji wengine ili kuvutia uwekezaji zaidi katika eneo hilo.
Aidha, ametoa wito kwa taasisi za Serikali kuunga mkono wawekezaji wa ndani kwa kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, ili kuimarisha mnyororo wa thamani, kulinda ajira na kuongeza mapato ya Serikali.
Kwa upande wake, Meneja wa TISEZA Kanda ya Ziwa, Phina Jerome, amesema Musumba Steel Tanzania Limited ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa wanaopata huduma na usaidizi wa karibu kutoka TISEZA, na amewahimiza wawekezaji wengine kuiga mfano huo kwa kuja kuchukua maeneo ya uwekezaji wilayani Kahama.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Uwekezaji Binafsi kutoka Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Fadhili Chilumba, amesema masuala ya uwekezaji yanaongozwa na Sheria ya Uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uchumi ya mwaka 2025, akisisitiza matumizi ya sheria sahihi ili kuvutia wawekezaji.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amesema ofisi yake inaendelea kuweka miundombinu wezeshi ili kuvutia wawekezaji pia watakuwa sababu ya wawekezaji kukua maana kupitia uwekezaji vijana watapata teknolijia, elimu, ajira na vitu vingine ambavyo vitakuwa chachu ya maendeleo yao binafsi na kwa taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Musumba Steel Tanzania Limited, Mdhibiti Ubora na Meneja wa Mradi wa kiwanda hicho, Andrew Samwel, amesema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2024 na hadi sasa kimeajiri wafanyakazi 65 na kuongeza kuwa uwekezaji huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 27, huku mpango ukiwa ni kuongeza uwekezaji huo hadi kufikia shilingi bilioni 35 ifikapo mwaka 2027.
Hata hivyo, ametaja changamoto ya ushindani wa bidhaa za chuma zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kwa bei ya chini, hali inayosababisha bidhaa za ndani kukosa soko.























No comments:
Post a Comment