Na Neema Nkumbi, Kahama
Hatimaye serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanikiwa kutatua changamoto sugu ya upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye ulemavu na mahitaji maalumu katika kata ya Segese, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, waliokuwa wakishindwa kuendelea na masomo kutokana na mazingira magumu ya maisha majumbani mwao.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ujenzi wa mabweni, nyumba ya matroni pamoja na uzio katika Shule ya Msingi Segese, miundombinu iliyolenga kuwahakikishia wanafunzi hao haki yao ya msingi ya elimu kwa kuwapatia mazingira salama, rafiki na yanayowawezesha kukaa shuleni na kuhudhuria masomo kwa wakati.
Akizungumza kuhusu manufaa ya mradi huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi Arafa Machambo, amesema ujenzi wa mabweni umeleta mapinduzi makubwa katika masuala ya mahudhurio na mwendelezo wa masomo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ambao awali walikuwa wakilazimika kukatisha masomo kabla ya kukamilisha elimu ya msingi.
“Sisi hapa tuna wanafunzi 14 wenye mahitaji maalumu. Dhumuni la kujenga mabweni haya ni kukusanya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Halmashauri ya Msalala, kwani kuna wazazi wengine wanawaficha watoto wao nyumbani kwa sababu hawawezi kuwaleta na kuwarudisha shuleni, Mabweni haya yatasaidia kuwaleta pamoja na kuwapatia haki yao ya elimu,” amesema Bi Arafa.
Kwa mujibu wa uongozi wa shule hiyo, umbali mrefu wa kutoka nyumbani kwenda shuleni, changamoto za kifamilia na kukosekana kwa uangalizi wa karibu vilikuwa miongoni mwa sababu kubwa zilizosababisha utoro na kuacha shule kwa wanafunzi wenye ulemavu, hali ambayo sasa imeanza kubadilika kufuatia ujenzi wa miundombinu hiyo.
Ujenzi wa mabweni hayo umeungwa mkono na wadau wa maendeleo, akiwemo Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambao umechangia ujenzi wa uzio na nyumba za wafanyakazi kwa lengo la kuhakikisha usalama na ustawi wa wanafunzi hao.
Meneja Uhusiano na Mazingira wa mgodi huo, Agapiti Paulo, amesema uamuzi wa kuwekeza katika mradi huo ulitokana na dhamira ya mgodi kusaidia jamii inayozunguka eneo la mgodi, hususan makundi yenye uhitaji maalumu.
“Tumeona umuhimu wa uwepo wa uzio na nyumba za wafanyakazi kwa ajili ya usalama wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Hii ni hatua muhimu kuhakikisha wanapata mazingira tulivu ya kujifunzia, Ujenzi huu umegharimu takribani shilingi milioni 300 hadi kukamilika,” amesema Agapiti.
Baadhi ya wanafunzi wanufaika wa mradi huo wameeleza furaha na matumaini mapya waliyonayo kufuatia uwepo wa mabweni, wakisema yatasaidia kufanikisha ndoto zao za kielimu bila hofu ya changamoto za usafiri na kurejea nyumbani kila siku.
“Uwepo wa bweni hili utatusaidia kutimiza ndoto zetu, kwani hata ambao hawakuwa na uwezo wa kufika shuleni sasa wataweza kusoma bila hofu ya nitarudije nyumbani,” amesema mmoja wa wanafunzi.
Akitoa kauli ya serikali wakati wa uzinduzi wa mabweni hayo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amewataka watendaji wa serikali na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wote wenye ulemavu na mahitaji maalumu wanatambuliwa, kuandikishwa shule na kupewa fursa sawa ya elimu kama watoto wengine.
“Changamoto ya watu wenye ulemavu ipo kwenye familia zetu, hivyo tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuwainua na kuwasaidia. Tuwaandikishe shule na vyuo vya ufundi. Nimekuja kuzindua bweni la watoto wenye ulemavu, lakini kazi hii si ya serikali pekee yake, ni jukumu la kila mmoja wetu, Serikali imewekeza sana katika sekta ya elimu,” amesema Mhita.
Ujenzi wa mabweni katika Shule ya Msingi Segese umeonekana kama mfano wa utekelezaji wa sera ya elimu jumuishi, unaolenga kuhakikisha hakuna mtoto anayenyimwa haki ya elimu kutokana na ulemavu au mazingira ya maisha, na hivyo kuendeleza dhamira ya serikali ya kujenga jamii yenye usawa na fursa kwa wote.





No comments:
Post a Comment