Na Neema Nkumbi, Kahama
Serikali imesema iko tayari kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mkandarasi Sichuan Road and Bridge Group (SRBG) anayetekeleza ujenzi wa barabara na mifereji ya maji katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, kufuatia utekelezaji usioridhisha na ukiukwaji wa masharti ya mkataba.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 15, 2026 na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia miundombinu katika Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Rogatus Matilila, wakati wa ziara ya ukaguzi na kufanya tathmini ya mradi huo huku akiambatana na timu ya wataalamu kutoka TAMISEMI wanaosimamia miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC).
Matilila amesema maendeleo ya ujenzi wa barabara na mifereji ya maji katika manispaa hiyo hayaridhishi licha ya mkandarasi kuongezewa muda mara kadhaa, huku kila wakati akiwasilisha maombi mapya ya nyongeza ya muda na kueleza kuwa muda wa mwisho wa nyongeza ya siku 230 unaishia leo Januari 15, 2026.
“Maendeleo ya kazi kwa mkandarasi huyu siyo ya kuridhisha kabisa, ameongezewa muda mara nyingi lakini mpaka sasa yuko nyuma sana, Tayari ameshakatwa fidia mpaka asilimia 100, lakini bado anaomba kuongezewa muda tena,” amesema Matilila.
Ameongeza kuwa timu hiyo imekagua barabara pamoja na mifereji ya maji ya mvua na kubaini utekelezaji wake kuwa wa kusuasua, ilhali mkandarasi huyo tayari amelipwa zaidi ya asilimia 20 ya thamani ya mkataba.
“Leo Januari 15 ndiyo mwisho wa muda alioongezewa hivyo tunakwenda kukaa kama timu, kupitia ripoti za mradi na masharti ya mkataba ili kufanya uamuzi sahihi; ama kuendelea na mkandarasi huyu au kuvunja mkataba na kumleta mkandarasi mwingine, ili kuwaondolea wananchi adha wanayoipata,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Matilila, baadhi ya sababu zinazotolewa na mkandarasi kujitetea ni za kujirudia na zisizo na uzito wa kutosha, ikiwemo changamoto ya mvua, uwepo wa maji kwenye eneo la mradi na upatikanaji wa lami.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, amekiri kuwepo kwa ucheleweshaji mkubwa wa mradi huo, hali inayowaathiri wananchi hususan kipindi cha mvua.
“Tumezunguka kwenye mradi huu tukiwa na wataalamu wetu, Kama Halmashauri na mwajiri, haturidhishwi na kasi ya utekelezaji wa mkandarasi huyu maana mpaka sasa ameweka lami kilomita moja tu kati ya kilomita 12 zinazotakiwa kufikiwa,” amesema Kibetu.
Wananchi wa Kahama nao wameeleza kuchoshwa na hali hiyo. Mkazi wa Kahama, Sofia Mbacha, akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameomba serikali kuchukua hatua kali dhidi ya mkandarasi huyo.
“Hizi barabara wanasema zinawekewa lami, lakini mitaro aliyochimba mkandarasi ni mikubwa sana, Mvua ikinyesha tunaishi kwa hofu, nyumba zinaweka nyufa, na baadhi zinaanguka na kama huna uwezo wa kuweka mifuko ya moramu kuzuia maji, basi unaumia, Wanafanya kazi kwa mwendo wa kinyonga,” amesema Sofia.
Hatua zitakazochukuliwa na serikali dhidi ya mkandarasi huyo zinatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa utekelezaji wa mradi huo muhimu, unaolenga kuboresha miundombinu na maisha ya wakazi wa Manispaa ya Kahama.




No comments:
Post a Comment