Na Neema Nkumbi, Kahama
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, ametoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara ndani ya Manispaa ya Kahama, kuhakikisha barabara zote zinapitika majira yote ya mwaka, hususan kipindi hiki cha mvua.
Maelekezo hayo yametolewa wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya miundombinu ya barabara na mitaro katika kata mbalimbali za manispaa hiyo, baada ya kuibuka kwa malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara, mitaro iliyoziba na hatari kwa usalama wa watoto na wakazi kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kukagua barabara ya Mtaa wa Mtakuja katika Kata ya Nyasubi, Ngayiwa ameiagiza TARURA kuwasimamia kwa karibu wakandarasi waliokabidhiwa miradi hiyo, akisisitiza kuwa fedha za utekelezaji tayari zimeshatolewa hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha au kufanya kazi isiyokidhi viwango.
“Baadhi ya barabara hizi zipo chini ya wakandarasi lakini bado zina mapungufu makubwa, natoa maelekezo kwa TARURA kuhakikisha wakandarasi wanasimamiwa kikamilifu, wafanye kazi kwa ubora na wakabidhi barabara kwa wakati,” amesema Ngayiwa.
Mbunge huyo amesema kuwa mandhari ya Manispaa ya Kahama ina maeneo mengi ya mabonde, hali inayosababisha maji ya mvua kuathiri kwa kiasi kikubwa miundombinu ya barabara endapo mitaro haitajengwa na kutunzwa ipasavyo.
Aidha, Ngayiwa amesisitiza kuwa barabara lazima ziweze kupitika katika vipindi vyote vya kiangazi na masika, ili wananchi waendelee kupata huduma muhimu kama elimu, biashara na afya bila vikwazo.
“Tunamwakilisha Mheshimiwa Rais kwa wananchi, ambaye anahangaika kutafuta fedha za maendeleo hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha fedha hizo zinaleta matokeo kwa wananchi kwa kusimamia wakandarasi kikamilifu,” ameongeza.
Katika maelekezo yake, Mbunge Ngayiwa pia ametoa wito kwa TARURA kuhakikisha mitaro yote iliyoziba kwa mchanga au takataka inafukuliwa ili kuruhusu maji kupita, hatua itakayosaidia kuzuia maji kukata barabara na kuingia kwenye makazi ya watu.
Hata hivyo, Mbunge huyo amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu kwa kutoziba mitaro kwa kutupa taka ovyo, akibainisha kuwa tabia hiyo inachangia uharibifu wa barabara na kuongeza madhara ya mafuriko.
“Serikali inaendelea kufanya juhudi kubwa kuboresha barabara, lakini kama wananchi hatutalinda miundombinu yetu, changamoto hizi zitaendelea kujirudia,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA wilaya ya kahama Mhandisi juma Masola amesema amepokea maelekezo ya Mbunge huyo na tayari amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara za Mhungolo Mbulu na Mtakuja Nyasubi kuhakikisha barabara hizo zinapitika haraka, huku mitaro ikifukuliwa ili kudhibiti mtiririko wa maji.
Ziara ya Mbunge Ngayiwa imeelezwa kuwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usalama wa wananchi, hususan watoto wanaoenda na kutoka shule, unalindwa wakati wa msimu wa mvua.
Mbunge Ngayiwa ametembelea kata ya Malunga, Majengo, Mhongolo, Nyasubi, Mhungula pamoja na Zongomela.




No comments:
Post a Comment