DATA NI DHAHABU: PDPC Sasa Kubana Makampuni ‘Yanaichezea’ Siri za Watanzania - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 23 January 2026

DATA NI DHAHABU: PDPC Sasa Kubana Makampuni ‘Yanaichezea’ Siri za Watanzania

 



TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) sasa inataka kuhakikisha kuwa kampuni hazichezei siri zako. Katika ulimwengu wa sasa wa TEHAMA, taarifa zako ni dhahabu. Kampuni nyingi zimekuwa zikitumia taarifa hizi kwa faida, wakati mwingine kuziuzia kampuni za matangazo au kuzisafirisha nje ya nchi bila wewe mwananchi kujua.

Hali hiyo imemlazimu Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, kutangaza kuanza kwa operesheni kabambe ya nchi nzima kufanya ukaguzi kwa taasisi za umma na binafsi ili kuona kama zinazingatia Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini , Dkt. Mkilia alisema hatua hiyo inakuja baada ya kumalizika kwa kipindi cha hiari ambacho taasisi zilipewa kurekebisha mifumo yao na kujisajili.

Uchambuzi wa mazingira ya sasa ya kidijitali nchini unaonyesha kuwa taarifa binafsi kama namba za simu, anuani za makazi, na rekodi za miamala zimekuwa bidhaa inayouzika. Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kupokea jumbe za matangazo au kupigiwa simu na watu wasiowajua, jambo linaloashiria kuwa siri zao zimevuja au zimeuzwa.

"Ukaguzi huu utahusisha kubaini taasisi zinazokusanya, kuhifadhi, kuchakata na kusafirisha taarifa binafsi nje ya nchi bila kuzingatia matakwa ya sheria," alisema Dkt. Mkilia na kuongeza:"PDPC tutachukua hatua kali, ikiwa ni pamoja na faini, kifungo, na kutoa fidia kwa waathirika dhidi ya kampuni au taasisi yoyote itakayokiuka sheria hii."




Hakuna ‘Mkubwa’ Mbele ya Sheria

Dkt. Mkilia ameweka msisitizo kuwa ukaguzi huo hautazingatia hadhi, ukubwa, wala umashuhuri wa taasisi. Lengo kuu ni kudhibiti mianya ambapo taarifa za Watanzania zinachakatwa na kusafirishwa kiholela bila ridhaa yao.

Kauli hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa teknolojia na wananchi wa kawaida, wengi wakisisitiza kuwa macho ya Tume yanapaswa kuelekezwa zaidi kwenye makampuni ya simu, mabenki, na taasisi ndogo za mikopo (Micro-finances) ambazo zimekuwa zikihusishwa na matumizi mabaya ya namba za wateja.

PDPC imekumbusha kuwa ifikapo Aprili 8, 2026, taasisi zote nchini zinapaswa kuwa zimekamilisha usajili na kuanza kuzingatia misingi ya ulinzi wa faragha za wananchi. Hatua hii si tu inalinda utu wa Mtanzania, bali pia inaiweka Tanzania katika viwango vya kimataifa vya usalama wa kidijitali.

Kwa sasa, mpira upo mikononi mwa wamiliki wa makampuni na wakuu wa taasisi, huku wananchi wakisubiri kuona kama kuanza kwa ukaguzi huu kutakomesha kero ya kupigiwa simu na wageni wanaojua siri zao kuliko inavyotarajiwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso