WATUHUMIWA SITA WAACHILIWA HURU NA DPP KAHAMA BAADA YA KUKOSA NIA YA KUENDELEA NA MASHTAKA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 2 December 2025

WATUHUMIWA SITA WAACHILIWA HURU NA DPP KAHAMA BAADA YA KUKOSA NIA YA KUENDELEA NA MASHTAKA




Na: Neema Nkumbi


Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kahama leo imawaachilia huru watuhumiwa sita waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuchoma mali na uharibifu wa mali, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutangaza kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.

Watuhumiwa hao Mohammed Mzungu, Ally Paulo, Peter Mhoja, Isaac Gerald, Dickson Mkoko na Godfrey Andrea walikuwa miongoni mwa watu tisa waliokamatwa kati ya Oktoba 29 na Novemba 4, 2025, wakihusishwa na vurugu zilizotokea kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kahama.
DPP Avuta Kesi Kwa Mujibu wa Sheria

Akitangaza uamuzi huo katika shauri namba 26513 la 2025, Wakili wa Serikali Salome Mbughuni aliieleza Mahakama kuwa DPP ametumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPC), Sura ya 20, marejeo ya 2023, kuondoa mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Christina Chovenye, aliridhia ombi hilo na kutangaza watuhumiwa hao kuwa huru.
Utetezi Wakubali Uamuzi, Waomba Upelelezi Kuharakishwa

Wakili wa Utetezi, Evodius Rwamgobe, alisema hawana pingamizi na uamuzi huo wa DPP na akaomba upelelezi kwa watuhumiwa waliobaki uharakishwe.


“DPP anayo mamlaka ya kufuta shauri lolote. Leo ametumia kifungu 92(1) na kutangaza hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya wateja wangu sita,” alisema Rwamgobe.
Furaha na Shukrani Baada ya Kuachiwa

Baadhi ya watuhumiwa waliotoka mahakamani hawakusita kuonyesha hisia zao za faraja.

Godfrey Andrea, mmoja wa walioachiwa, alisema:


“Walinikamata nikiwa Lumambo stendi nikielekea kuchukua mahitaji. Leo wameona sina hatia na wameniachia. Naitumia nafasi hii kuishukuru sana serikali yangu.”

Aidha, Regina Rutege mzazi wa mmoja wa vijana walioachiwa alitoa shukrani kwa serikali huku akiiomba iwatazame pia vijana wengine waliobaki rumande.


“Kukamatwa kwa watoto wangu kumeniathiri sana. Mimi ni mjane, namlea mama mkwe wangu mwenye uvimbe wa kansa kitandani kwa mwaka wa sita. Nawaomba serikali iwaangalie na wale waliobaki,” alisema.

Uamuzi wa DPP umeleta nafuu kwa familia zilizokuwa zikikabiliwa na msongo wa mawazo huku zikiendelea kusubiri mustakabali wa watuhumiwa wengine watatu ambao shauri lao bado linaendelea.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso