WASIMAMIZI WA MRADI WA SHULE HATARINI, MKUU WA MKOA AAGIZWA KUWAKAMATA NA KUWAHOJI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 15 December 2025

WASIMAMIZI WA MRADI WA SHULE HATARINI, MKUU WA MKOA AAGIZWA KUWAKAMATA NA KUWAHOJI





OWM- TAMISEMI,Mtwara


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, ameagizwa kuwakamata na kuwahoji wahusika wa usimamizi wa mradi wa Shule ya Sekondari ya Amali Makondeni, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, kufuatia tuhuma za usimamizi mbovu wa mradi huo.


Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Shemdoe, mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo.


Mhe. Kwagilwa amesema mradi huo umetumia zaidi ya shilingi milioni 464 bila kukamilika, huku ukihitaji shilingi milioni 48 za ziada kwa ajili ya kukamilishwa. Hali hiyo ameieleza kuwa ni kinyume na maelekezo ya Serikali na inaashiria uzembe pamoja na uwezekano wa upotevu wa fedha za umma.


“Ninamwelekeza Mkuu wa Mkoa kufuata taratibu zote za kisheria na kutumia mamlaka aliyonayo kuwakamata na kuwahoji wahusika wa mradi huu kwa tuhuma za upotevu wa shilingi milioni 48,” amesema Mhe. Kwagilwa.


Aidha, baada ya kubaini dosari za kiusimamizi katika utekelezaji wa mradi huo, Naibu Waziri huyo amemuagiza Katibu Mkuu wa OWM–TAMISEMI kuhakikisha ndani ya siku 21 anapelekwa Mkuu wa Idara ya Ujenzi katika halmashauri husika, ili kuimarisha usimamizi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso