Tanzania Bloggers Network (TBN) leo imetoa salamu za pongezi kwa Watanzania wote katika maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru, ikisisitiza umuhimu wa kutafakari safari ya Taifa na wajibu wa kuendeleza msingi wa amani, utulivu na maendeleo.
Katika taarifa yake, TBN imesema kuwa Uhuru si tukio la kihistoria pekee, bali ni mwendelezo wa jukumu la kujenga Taifa imara, ikinukuu kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusisitiza kuwa Uhuru haukamiliki bila kujitegemea na kufanya kazi kwa bidii.
TBN imeonya kuwa vurugu na uchochezi vinaweza kudhoofisha juhudi za kupambana na maadui watatu—ujinga, umaskini na maradhi—kama ilivyoasisiwa tangu enzi za uhuru. Imenukuu pia kauli ya Rais mstaafu Benjamin William Mkapa aliyehimiza kuwa amani si jambo la kutokea bali inahitaji kulindwa kila siku.
Mtandao huo umeongeza kuwa kila kizazi kina wajibu wa kuendeleza gurudumu la maendeleo, ukikumbusha kauli ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kwamba kila utawala una zama na mchango wake katika ujenzi wa Taifa.
TBN imesema kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchi inaendeleza dira ya 4R—Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya—na kuwataka Watanzania kuunga mkono mwelekeo huo kwa kutumia uhuru wa maoni kujenga badala ya kubomoa.
Ikihitimisha salamu zake, TBN imetoa wito kwa wananchi kuthamini Uhuru kwa kudumisha amani, kufanya kazi kwa bidii na kukataa kutumiwa katika shughuli zinazoathiri umoja wa Taifa.
Mtandao huo umewatakia Watanzania maadhimisho mema ya miaka 64 ya Uhuru, ukisisitiza kaulimbiu yake: “TANZANIA KWANZA, KAZI NA UTU TUSONGE MBELE.”

No comments:
Post a Comment