NA NEEMA NKUMBI, KAHAMA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewataka Madiwani wa Manispaa ya Kahama kuhakikisha mapato ya manispaa yanaongezeka na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ili wawe mfano kwa halmashauri zingine huku akisisitiza kuwa maendeleo ya wananchi yanategemea ufanisi wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
Mhe. Mhita ametoa wito huo mapema leo wakati wa mkutano wake wa kwanza na Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kahama tangu kuchaguliwa kwa madiwani hao Oktoba 29, 2025, Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Kahama, ukihusisha pia wataalamu wa halmashauri na viongozi wa kisiasa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa amesema kipimo halisi cha utendaji kazi wa viongozi ni uwepo wa huduma bora za kijamii na miundombinu imara, akibainisha kuwa mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mapato ya kutosha yanayotokana na makusanyo ya ndani.
“madiwani muhakikishe mapato ya ndani yanaongezeka kwani mkiwa na fedha za kutosha mtaweza kutatua changamoto za ndani kama ujenzi wa barabara, upatikanaji wa mapato ya asilimia na fedha ndizo zitaamua ubora wa huduma tunazotoa kwa wananchi,” amesema Mhe. Mhita.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mawasiliano kati ya Madiwani, wataalamu, wananchi na vyombo vya habari, akionya dhidi ya kauli zinazokinzana ambazo huathiri uaminifu wa Serikali kwa wananchi, ambapo ameeleza kuwa kauli moja yenye uelewano wa pamoja ndiyo msingi wa kujenga imani na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mhita amewataka wataalamu wa Manispaa ya Kahama kuepuka kujenga matabaka baina yao, badala yake wafanye tathmini ya utendaji wao na kuwajibika ipasavyo ili kuwa wepesi wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
" Wakuu wa idara kila mtu ajifanyie tathimini kwani hatuko tayari kuichonganisha serikali na wananchi tutachukua hatua kwa wote watakaosababisha vikwazo vya maendeleo ya wananchi", amesema.
Katika wito wake kwa Madiwani, Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, mshikamano na uwajibikaji, akieleza kuwa mafanikio ya Manispaa ya Kahama yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa dhati kati ya viongozi wa kisiasa na watendaji.
“Nawasihi muendelee kushikamana kwani Umoja, mshikamano na uwajibikaji ni silaha yetu kubwa ya kufanikisha mipango ya maendeleo, Tukitanguliza maslahi ya wananchi na ajenda za pamoja, tutaleta mabadiliko makubwa Kahama,” amesisitiza.
Pia amewahimiza Madiwani kuhakikisha wanawasilisha taarifa sahihi za changamoto za wananchi katika maeneo yao kwa Halmashauri, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati, sambamba na kushiriki kikamilifu katika kubuni na kusimamia vyanzo vipya vya mapato.
Mhe. Mhita ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuwa daraja la mafanikio kwa kuhakikisha maazimio yote ya Baraza la Madiwani yanatekelezwa kwa weledi, kwa lengo la kujenga na kudumisha imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kahama, Mhe. Matuluma Kaniki, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara hiyo, akisema imewapa Madiwani ari na hamasa mpya ya kuendelea kuwatumikia wananchi kwa bidii, weledi na ushirikiano wa karibu na Serikali Kuu.
Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mkoa wa Shinyanga wa kuimarisha uhusiano kati ya viongozi wa kisiasa na watendaji wa Serikali, kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo katika halmashauri zake na hatimaye kurejesha tabasamu kwa wananchi.








No comments:
Post a Comment