MWANAFUNZI ALIYEKOSA MTIHANI KWA KUKAMATWA KUFUATIA VURUGU ZA MAANDAMANO YA OKTOBA 29, SASA AACHIWA HURU - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 1 December 2025

MWANAFUNZI ALIYEKOSA MTIHANI KWA KUKAMATWA KUFUATIA VURUGU ZA MAANDAMANO YA OKTOBA 29, SASA AACHIWA HURU



Macho yenye mchanganyiko wa faraja na masikitiko yametawala uso wa Philipo Kasanda, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kakola, baada ya mahakama ya Wilaya ya Kahama kusoma kuwa hana tena mashitaka yaliyokuwa yakimkabili na yaliyomnyima nafasi ya kufanya mtihani wa taifa wa upimaji.

Katika uamuzi uliosomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwanaidi Mtemi, Wakili Mwandamizi wa Serikali Jukael Jairo ameeleza kuwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) ameondoa shauri namba 26543 akitumia mamlaka yake chini ya kifungu 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Uamuzi huo uliwanufaisha watuhumiwa tisa waliokamatwa Oktoba 29 wakati wa maandamano yaliyodaiwa kuwa hayakuwa na kibali.

Kwa Philipo, siku hii imekuwa zaidi ya kuachiwa tu kwani imekuwa siku ya kurejea kwenye ndoto alizodhani zimefifia.


“Nataka tu kurudi shule, Nimekosa mtihani muhimu sana, Nawaomba wazazi wangu wanisaidie nisiache masomo,” amesema kwa sauti ya unyenyekevu, akieleza namna alivyokuwa akihesabu siku tangu akamatwe Novemba 4.

Watuhumiwa wenzake akina John Maduka, Issa Miraji, Emmanuel Magina na wengine, waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka matano kama kuchoma moto majengo na unyang’anyi wa kutumia silaha, wamepeana mikono nje ya mahakama wakionesha hisia za kupata pumzi mpya baada ya wiki kadhaa za hofu na sintofahamu.

Wakili wa utetezi Evodius Rwamgobe amesema uamuzi wa DPP ni nafasi kwa vijana hao kujitathmini upya.


“Ni nafasi kwao kujenga upya maishaSheria imeruhusu, na sisi tumepokea kwa mikono miwili,” amesema.

Kwa upande wake, Issa Miraji, mmoja wa waliokuwa wakishtakiwa, amesema tukio hilo limekuwa funzo kubwa kwake na kwamba sasa atatumia sauti yake kuwashauri vijana kuepuka misukumo inayoweza kuwaingiza kwenye hatari zisizokuwa za lazima.


“Nataka kuwa balozi wa amani, Vijana tunapaswa kufikiri mara mbili kabla ya kushiriki matukio yanayoweza kutuvurugia maisha,” amesema.

Kwa jamii ya Kahama, kuachiwa kwa watuhumiwa hawa sio tu kufungwa kwa jalada la shauri bali pia ni kioo kinachowaonesha namna matukio madogo yanavyoweza kuathiri mustakabali wa maisha, hasa ya vijana wanaojenga ndoto zao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso