Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Glory Absalum, akizungumza wakati wa kufungua kikao cha baraza la madiwani ambapo amewasisitiza madiwani hao kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI
Meya wa Manispaa ya Kahama Mataluma Kaniki, akizungumza leo disemba 2, 2025, mbele ya baraza la madiwani hukuakiwashukuru madiwani kwa kumchagua
Na Neema Nkumbi, Kahama
Baraza la kwanza la madiwani wa Manispaa ya Kahama limefanyika leo disemba 2, 2025 ambapo viongozi mbalimbali wamewataka madiwani hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya sheria na maadili ya utumishi wa umma.
Akifungua kikao hicho, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum, amewataka madiwani kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, huku akisisitiza kuwa uongozi wa halmashauri unategemea ushirikiano, uwajibikaji na uadilifu kutoka kwa kila diwani.
Katika hatua nyingine, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Mhe. Hussein Salum, amewaongoza madiwani hao katika zoezi la kula kiapo cha udiwani, Hakimu huyo amewakumbusha kuzingatia kiapo walichoapa kwa kufanya kazi kwa haki, uaminifu na kusimamia maslahi ya wananchi.
Aidha, madiwani hao walikula kiapo cha maadili kilichoongozwa na Afisa wa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Umma Kanda ya Tabora, Halima Ramadhan, ambaye amewakumbusha umuhimu wa kufuata misingi ya maadili ya viongozi wa umma na kuepuka vitendo vinavyoweza kukiuka maadili ya uongozi.
Katika kikao hicho, madiwani wa 28 wa kata 20 za Manispaa ya Kahama pamoja na viti maalum wameapishwa rasmi, hatua inayofungua ukurasa mpya wa uongozi katika halmashauri hiyo Sambamba na kuapishwa kwa madiwani, uchaguzi wa viongozi wa baraza umefanyika ambapo Mataluma Kaniki, Diwani wa Kata ya Nyasubi, amechaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Kahama, Vilevile Shabani Mikongoti, Diwani wa Kata ya Mwendakulima, amechaguliwa kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri Manispaa ya Kahama, Laurent Kwabi, amesema: “Sisi kama wazee tunatarajia mafanikio makubwa kwenye baraza hili la madiwani, Pia nawasihi madiwani wanapoenda kutatua kero za wananchi waangalie sana kero za vijana.”
Wakizungumza baada ya kuchaguliwa, Meya na Naibu Meya wameomba ushirikiano baina yao na wataalamu wa halmashauri kwa maslahi ya wananchi, Naibu Meya ameongeza kuwa changamoto kubwa inayowakabili vijana ni ajira, hivyo ni muhimu viongozi kuwa waadilifu na waaminifu ili kuhakikisha vijana wanapata majawabu ya changamoto hizo.
Mzee Kwabi ameongeza kuwa serikali inatoa fedha za mikopo kwa ajili ya vijana, hivyo wanapaswa kupewa elimu na mikopo kulingana na shughuli zao mfano dereva bajaji kupewa mkopo wa bajaji, na mkulima kupewa mkopo unaolingana na kazi yake.
Naye Diwani wa Viti Maalum, Tarafa ya Isagehe, Mpaji Mwalimu, amesema atasimama na vijana pamoja na wanawake kuhakikisha wananufaika na mikopo mbalimbali ya halmashauri, Pia amesema ana imani kuwa Meya na Naibu Meya watasimama na wananchi na kutatua changamoto zao kwa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri.
Baraza hilo linaashiria kuanza rasmi kwa majukumu ya madiwani wapya katika kuisimamia, kuongoza na kuiendeleza Manispaa ya Kahama, huku wananchi wakitarajia uwajibikaji, umoja na utekelezaji wa miradi yenye tija kwa jamii.
















No comments:
Post a Comment