DC NKINDA AKUTANA NA VIJANA KAHAMA KUSHEREHEKEA SIKUKUU YA XMAS, ASIKILIZA KERO NA KUWAHIMIZA KULINDA AMANI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 25 December 2025

DC NKINDA AKUTANA NA VIJANA KAHAMA KUSHEREHEKEA SIKUKUU YA XMAS, ASIKILIZA KERO NA KUWAHIMIZA KULINDA AMANI



Na Neema Nkumbi, Kahama



MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, amekutana na makundi mbalimbali ya vijana wilayani humo katika hafla ya pamoja ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, iliyolenga kuimarisha mshikamano kwa kula chakula cha pamoja sambamba na kusikiliza changamoto zinazowakabili vijana wa Kahama.

Akizungumza katika mkutano huo, Mchungaji wa Kanisa la Kalvari Lango la Ushindi, Mchungaji Flora Mwanri, amempongeza Mhe. Nkinda pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya Glory Absalum kwa hatua ya kuwakutanisha wananchi wa Kahama bila kujali dini au itikadi za kisiasa kwani tukio hilo limeonesha mfano wa uongozi unaojali umoja na mshikamano wa jamii, akibainisha kuwa kiongozi huyo amewaunganisha wananchi wote kwa pamoja.

Kwa upande wake, kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo wilayani Kahama, Abas Omari, amewasilisha kero kadhaa ikiwemo ombi la kuwekwa taa za barabarani katika eneo la Shunu ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kibiashara nyakati za usiku, Pia ameeleza changamoto ya barabara ya kuelekea makaburini ya Shunu ambayo huwa haipitiki wakati wa mvua kutokana na tope, hali inayowalazimu baadhi ya wananchi, wakiwemo waliovaa kanzu, kuzikunja ili kupita.

Aidha, ameeleza kuwa barabara ya eneo la Msikiti wa Shunu Lugela imekatika kabisa, jambo linalowalazimu watoto wanaotoka upande wa pili kuzunguka milimani kufika Shule ya Msingi Shunu.

Akitoa nasaha zake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Kahama (OCD), Mtaju, amewataka wananchi na vijana kutokuwa na hofu ya kufikisha changamoto zao polisi wakati wowote amesema ofisi yake iko wazi muda wote na endapo changamoto itahitaji utatuzi wa ngazi za juu, atalifikisha kwa mamlaka husika.

Pia, amewahimiza vijana kutumia hekima katika kutatua changamoto, akisisitiza kuwa vijana ni nguvu kazi na tegemeo la taifa, hivyo wanapaswa kuepuka kujihusisha na shughuli zisizo halali zinazoweza kukatiza ndoto zao.

Akijibu hoja na kero zilizowasilishwa, Mhe. Nkinda amesema kuhusu barabara ya makaburini Shunu, amemtaka aliyetoa changamoto hiyo kufika ofisini kwake kufikia Jumatatu ili yeye na timu ya wataalamu wa wilaya waende eneo husika kujionea ukubwa wa tatizo na kulifanyia kazi kwa haraka.

Kutokana na vijana wengi kuwa na changamoto amesema wataandaa kongamano maalum la vijana, litakalowapa fursa ya kuwasilisha changamoto zao kwa kina ili zipatiwe ufumbuzi.

Mhe. Nkinda amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina utaratibu wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi, iwe ni kwa makundi au mtu mmoja mmoja, akibainisha kuwa milango ya ofisi yake iko wazi kwa wananchi wote.

Katika hitimisho lake, Mkuu wa Wilaya aliwataka vijana wa Kahama kuendelea kuwa watulivu, kulinda amani na mshikamano, akisisitiza kuwa uongozi wa wilaya uko pamoja nao katika kuhakikisha maendeleo na ustawi wa wananchi wa Kahama yanaendelea kupatikana.

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso