AMANI HAIIMBIWI VINYWANI TU:WITO WA KUISHI AMANI MIOYONI NA KUWAJIBIKA KITAIFA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 14 December 2025

AMANI HAIIMBIWI VINYWANI TU:WITO WA KUISHI AMANI MIOYONI NA KUWAJIBIKA KITAIFA


Amani haimbiwi vinywani tu: Wito wa kuishi amani mioyoni na kuwajibika kitaifa


Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Said Miraji, ametoa wito kwa Watanzania, akisema amani ya kweli inapaswa kuwa zaidi ya kaulimbiu; inapaswa kuwa mtindo wa maisha unaoongozwa na matendo chanya na uwajibikaji.


Akizungumza katika mdahalo wa Athari za Kiuchumi Zitokanazo na Vurugu za Chaguzi Barani Afrika, Bw. Miraji alisisitiza, “Hatuwezi kuwa wamoja na kuimba amani vinywani tu; badala yake, tunapaswa kuiishi amani mioyoni mwetu na kuitendea kazi kupitia matendo yetu.”


Miraji alibainisha formula rahisi lakini yenye nguvu ya kujenga umoja wa kitaifa, akisema: “Umoja unajengwa kwa imani, imani inajengwa kwa usawa, na usawa unajengeka kwa kushirikiana.”


Alieleza kuwa ni kupitia usawa huo, ambapo wananchi wote wanahisi thamani yao inatambulika, ndipo watajenga imani ya kweli kwa serikali na kushikamana, na hivyo kuishi katika taifa lenye amani na mabadiliko chanya.


Mchambuzi huyo alielekeza jukumu kubwa kwa viongozi na wazee katika kulinda amani, hasa kwa kuweka mfano mwema. Amesema wazee wanapaswa kutumia hekima katika kuishi, kwani kwa mfano wao vijana wataweza kuelewa vyema na kuiga, na hivyo kuwasahihisha wale ambao bado hawajaufahamu vyema athari za vurugu na utengano. Uelimishaji huu kupitia matendo unatajwa kuwa njia bora ya kujenga jamii yenye utulivu.


Pia Bw. Miraji alisisitiza kuwa jukumu la amani halimaliziki kwa raia pekee. Alitoa wito kwa serikali kuanza kwa kuhakikisha inawawajibisha viongozi wasiokuwa watendaji.


"Hatua hii itapunguza changamoto katika jamii zinazosababishwa na kukosekana kwa mahitaji muhimu," alisema. Uwajibikaji huo unatarajiwa kusaidia kuepusha ongezeko la watu wanaokumbwa na matatizo ya kijamii, na kuchangia katika utatuzi wa masuala mbalimbali kabla hayajasababisha mifarakano au kutokuaminiana.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso