Athari za uchochezi na vurugu za kisiasa zimeonekana wazi nchini, huku wananchi wakijifunza somo gumu kuhusu thamani ya amani. Sauti za maumivu na majuto sasa zimegeuka kuwa wito wa umoja, huku vijana wakihimizana kujiepusha na habari za uchochezi na kuelekeza nguvu zao kwenye shughuli za uzalishaji.
Bi. Faudhia Ramadhani, mkazi wa Chanika, ni miongoni mwa wananchi waliohisi maumivu ya machafuko hayo, akitoa ushahidi wa athari hizo.
“Kilichotokea sitamani tena kijirudie. Tunapenda tuwe na amani, hatutaki tena itokee kama ilivyotokea. Tumeona kilichotokea, tumehisi maumivu, na sasa tumejifunza,” ameeleza Faudhia.
Kauli yake inaunga mkono hisia za Watanzania wengi, ambao wamekiri kwamba uwepo wa vurugu kipindi cha uchaguzi ulipelekea wananchi kuwa na hofu, kukimbia biashara zao na makazi yao, na kupoteza baadhi ya mali na kukosa mahitaji muhimu ya kila siku kwa siku kadhaa.
“Vurugu zimewaumiza wananchi,” alisema mmoja wa wachangiaji, akisisitiza kuwa amani ni maendeleo.
Faudhia Ramadhani ametoa wito mzito kwa vijana wenzake, akihimiza kipaumbele kipya cha maisha: kazi badala ya machafuko.
“Nawashauri vijana wenzangu tusijihusishe na machafuko yoyote yale. Wito wangu ni tufanye kazi tuachane na habari za uchochezi,” amesisitiza Faudhia.
Ujumbe huu umepokewa vyema na vijana wengine, ambao wamekiri kuwa ni jukumu lao kulinda amani. Kauli mbiu mpya imejitokeza: “Tufanye Kazi, Si Kelele; Tanzania Inahitaji Maendeleo, Si Maandamano.”
Wananchi mitandaoni na katika vijiwe mbalimbali wanakumbushana kuwa, ingawa vurugu ilichoma mali, haikuweza kuchoma roho ya Tanzania. “Leo tunasimama tena, tukiwa wamoja, tukiitazama amani kama mwanga wa kesho yetu,” walisema.
Vijana wanakumbushwa kuwa amani hii inatakiwa kulindwa kwa wivu mkubwa na kwamba wao ndio dhamana ya taifa hili. Wanahimizana kuendelea kuwa mstari wa mbele kuhubiri amani kupitia maridhiano.
Kama Faudhia anavyosisitiza, vijana wajiepushe na vyanzo vyote vya habari vinavyolenga kuchochea chuki na kugawanya taifa, ili kulinda msingi wa amani ambao ni muhimu kwa maisha na maendeleo yao binafsi na ya nchi kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment