
Viongozi wa Taasisi 22 za Kiislamu nchini Tanzania, wakiongozwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir bin Ally, wametoa tamko kali la kulaani vurugu zilizotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Pamoja na tamko hilo wameeleza bayana kuwa wanaunga mkono kikamilifu hatua za serikali za kurejesha utulivu na kuanzisha maridhiano ya kitaifa.
Tamko hilo lilitolewa baada ya viongozi hao kumaliza ibada maalum ya Itikafu iliyofanyika katika Msikiti wa Mfalme Mohammed wa Sita, Makao Makuu ya BAKWATA.
Madhumuni ya Itikafu hiyo ilikuwa ni kumkimbilia Mwenyezi Mungu, kutoa dua kwa waliofariki na walioathirika, na kutafakari njia sahihi ya kuipeleka nchi mbele baada ya matukio mazito ya uchomaji nyumba, vituo vya mafuta, uharibifu wa miundombinu, na kusababisha vifo vya raia na askari.
Viongozi hao wamesisitiza kwamba wamehuzunishwa sana na hali iliyotokea, ikiathiri taswira ya nchi, na wamelaani matamko yaliyotolewa na baadhi ya watu au vikundi yenye kuchochea hasira na kuharibu amani.
Maazimio Makuu Yaliyotangazwa:
1. Kuunga Mkono Rais Samia: Taasisi hizo zimepokea kwa heshima na kuunga mkono Hotuba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni mnamo Novemba 14, 2025.
2. Tume Huru na Maridhiano: Wameunga mkono hatua ya Rais ya kuunda Tume Huru ya Uchunguzi (Enquiry Commission) kubaini kiini cha tatizo, ambayo taarifa yake itatumika kuongoza mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa.
3. Maridhiano Siyo Kichaka cha Uhalifu: Ingawa wanaunga mkono maridhiano, wameonya kuwa mchakato huo usitumike kuficha uhalifu. Wamesisitiza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kina, usio na upendeleo, kubaini waliochochea, kupanga, na kuratibu uhalifu huo ili haki isimame sawa.
4. Wito kwa Vijana na Watanzania: Taasisi za Kiislamu zimewataka Waislamu na Watanzania wote kudai haki zao kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa, na wamekataa mijadala ya mitandaoni inayoeneza chuki za kidini, kikabila, au kikanda. Wamefika mbali kwa kuwasihi vijana kuitumia tarehe 9 Desemba kukaa nyumbani na wazazi wao kwa ajili ya kuombea taifa na kuepuka mikusanyiko inayoweza kusababisha vurugu.
Taasisi hizo pia zimeahidi kuwa daraja la kuunganisha Watanzania na zimeitaka Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma waliofiwa na walioharibikiwa na mali zao. Mufti ametoa wito kwa Waislamu kutumia kauli za kujenga na kuleta umoja.
No comments:
Post a Comment