TANZANIA YATHIBITISHA ULIMWENGUNI: NCHI IKO SALAMA KWA UTALII NA UWEKEZAJI — DKT. ABBASI ATOA KAULI RIYADH - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 10 November 2025

TANZANIA YATHIBITISHA ULIMWENGUNI: NCHI IKO SALAMA KWA UTALII NA UWEKEZAJI — DKT. ABBASI ATOA KAULI RIYADH


Na Mwandishi Wetu, Riyadh


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, ameuaminisha ulimwengu kwamba hali ya utalii na amani nchini Tanzania ni imara na waje watembee na kuwekeza.


Ametoa kauli hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa 26 wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), ulioanza Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia, kufuatia vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi katika baadhi ya maeneo.


Alisema hayo akichangia Ripoti ya Mwaka ya Utekelezaji ya shirika hilo, ambapo Tanzania pia ilinufaika na programu mbalimbali, ikiwemo kuandaa Mkutano wa Kanda ya Afrika wa Utalii wa Chakula (Gastronomy Tourism) uliofanyika Arusha mwezi Aprili, pamoja na ufadhili wa baadhi ya programu za uhifadhi wa mazingira katika Milima ya Usambara.


“Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza hili, baada ya kumpongeza Katibu Mkuu na Sekretarieti ya UN Tourism kwa utekelezaji ambao pia Tanzania imenufaika nao, nitumie fursa hii kuripoti kwamba Tanzania iko salama kufuatia tukio lililotokea wakati wa uchaguzi.


“Serikali imefanya jitihada na kurudisha nchi yetu katika hali ya utulivu, na hivyo kuhakikisha inabaki salama kwa watalii, na vivutio vyetu vyote, ambavyo mnajua, viko salama. Ninakaribisha wajumbe wa Mkutano huu na wadau wengine wa utalii kuja na kuendelea kutembelea nchi hii, ambayo ni kivutio bora zaidi Afrika kwa utalii wa safari,” alisema Dkt. Abbasi.


Aidha, mbali na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 32 tu kati ya wanachama 160 wa Shirika hilo, kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Utekelezaji (Executive Committee), Mkutano Mkuu huo pia uliidhinisha Tanzania kuwa Mjumbe wa Kamati ya Hati za Utambulisho (Credentials Committee) ya UN Tourism.


Mkutano huo pamoja na mambo mengine, unajadili matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) katika kukuza utalii. Pia mkutano huo ulimthibitisha Sheikh Nasser Al Nowais kutoka UAE kama Katibu Mtendaji mpya wa taasisi hiyo muhimu kwa sekta ya utalii duniani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso