Na Neema Nkumbi, Kahama
Mzee Hamis Mgeja, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, amezikwa leo novemba 4, 2025 katika makaburi ya Waislamu wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Katika mazishi hayo yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, chama na taasisi za dini, viongozi wamemsifu marehemu kwa mchango wake mkubwa katika siasa na malezi ya viongozi wengi nchini.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, akizungumza kwa niaba ya wanachama wa CCM mkoani humo, amesema Mzee Mgeja alikuwa kiongozi mpenda watu, mwenye msimamo wa kweli na mwalimu wa siasa kwa watu wengi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, katika salamu zake za rambirambi, amesema “Nimemfahamu tangu tukiwa vijana, alikuwa mfano wa kuigwa kwa wote, Tuna wajibu wa kumshukuru Mungu na Rais Samia, kwani leo tumeweza kukutana pamoja kumuenzi.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema marehemu alikuwa karibu naye kila siku kwa mazungumzo yaliyolenga kumjenga na kumshauri kwa hekima.
Viongozi mbalimbali waliotoa salamu za rambirambi ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, RPC wa Mkoa wa Geita, Sophia Jongo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha na wengine wengi.
Kutoka Ikulu, wawakilishi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rajab na Abdala Bulembo, walihudhuria kutoa salamu za pole kwa niaba ya Rais.
Viongozi wa dini nao hawakusita kutoa wito kwa wananchi kumrudia Mwenyezi Mungu na kuendeleza amani na upendo aliohubiri marehemu. Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, aliyewakilisha Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, pamoja na Mwenyekiti wa BAKWATA Taifa, ametoa salamu za rambirambi kwa niaba ya taasisi hiyo ya kiislamu.
Mzee Hamis Mgeja atakumbukwa kama kiongozi mzalendo, mpenda haki, na mwalimu wa siasa ambaye alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya chama na taifa kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment