MKUU WA WILAYA YA KAHAMA AONGOZA KIKAO CHA WENYEVITI KUIMARISHA AMANI NA UWAWIBIKAJI KATIKA JAMII - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 24 November 2025

MKUU WA WILAYA YA KAHAMA AONGOZA KIKAO CHA WENYEVITI KUIMARISHA AMANI NA UWAWIBIKAJI KATIKA JAMII


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, ameongoza kikao kazi na Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, katika mkutano maalum uliolenga kuhimiza umoja, uwajibikaji na kuimarisha AMANI katika jamii.


Kikao hicho kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kimejumuisha viongozi wa ngazi ya chini ambao ndio kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, wakipewa maelekezo ya namna ya kuendelea kusimamia utulivu na kushughulikia kero za jamii kwa haraka na ufanisi.


Akizungumza kwenye kikao hicho, Mhe. Nkinda amesisitiza kwamba viongozi wa mitaa na vijiji wana nafasi kubwa katika kudhibiti migogoro, kuhamasisha maelewano sambamba na kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi. Amesema kuwa Serikali inaamini kazi yao ni msingi wa amani ya kudumu.


*Amani inaanzia chini. Wenyeviti ni macho na masikio ya Serikali. Tunahitaji muendelee kuwa mstari wa mbele kuimarisha ushirikiano, kutatua changamoto za wananchi mapema na kuhakikisha jamii inabaki yenye utulivu*, amesema Mhe. Nkinda.


Aidha, ametoa rai kwa viongozi hao kuhakikisha kero zinazowasumbua wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi, ulinzi, na masuala ya kijamii zinafikishwa mara moja katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili zipatiwe ufumbuzi wa pamoja na kwa wakati


Kwa upande wao, Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji wamepongeza uongozi wa wilaya kwa kuwashirikisha moja kwa moja katika mijadala ya maendeleo na masuala yanayogusa ustawi wa wananchi. Wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali, kuhakikisha kila changamoto inashughulikiwa kwa uwazi na busara.


Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano ya kuongeza nguvu katika ulinzi shirikishi, kutoa elimu ya amani kwa wananchi, na kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa mitaa na wadau mbalimbali, ili kuifanya Kahama iendelee kuwa wilaya salama, yenye mshikamano na mwelekeo mzuri wa maendeleo.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso