Mkoa wa Mbeya umerejea katika utulivu kamili huku shughuli za kibiashara na kijamii zikichukua kasi, kufuatia siku chache za vurugu za kisiasa zilizogharimu maisha na mali. Kurejea huku kwa hali ya kawaida kumeambatana na sauti za wananchi zilizojawa majuto na msisitizo mkubwa wa thamani ya amani na utulivu.
Wananchi wa Mbeya, ambao wengi wao hutegemea mapato ya kila siku, wameeleza jinsi vurugu hizo zilivyowaathiri moja kwa moja.
Tuli Kyando, mfanyabiashara mkazi wa Uyole, amesema vurugu zimeacha vilio na hasara kubwa kwa wafanyabiashara. “Siku tatu tulizokaa nyumbani zimenigharimu sana kibiashara. Maisha ya Mtanzania ni kutoka na kutafuta chakula cha siku hiyo,” ameeleza Kyando.
Amesisitiza kuwa vitendo walivyofanya vijana vilikuwa si vizuri, kwani vimeharibu uwekezaji ambao ni ajira za watu kwa kuchoma moto mali zilizokuwepo. Amewataka vijana kuacha kutumia hasira na badala yake waone namna bora ya kufanya mambo, ikiwemo kukaa chini na kuzungumza.
Naye Nico Lawio Njowela, mkazi mwingine wa Mbeya, amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria. “Kwa sisi vijana, tunapokuwa na changamoto za maisha, ni vizuri tukafanya mambo kwa kufuata viongozi na sheria ili kupata suluhisho, kuliko kuchukua sheria mkononi. Watanzania ambao tuna hali ya chini tuliteseka sana kwenye hii vurugu,” amesema Njowela.
Kufuatia hasara hiyo, jumbe za wananchi mitandaoni zimejikita katika kukataa uchochezi na kuwataka Watanzania waungane kulinda nchi yao. Wengi wamehoji mantiki ya vurugu wakisema inafaidisha wachache tu.
“Maandamano ni biashara, wachache inawalipa na kuwanufaisha zaidi huku wengi tukiumia kwa kupoteza kazi, biashara zetu na madhara mengine mengi,” alieleza mmoja wa wajasiriamali.
Wananchi wamesisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kamwe kuharibu amani. Wamekariri msemo kuwa, “Amani huleta fursa kwa vijana na maendeleo; tuzidi kuwa imara katika kulinda Amani ya nchi yetu.”
Katika kuendeleza umoja, ujumbe mkuu wa wananchi ni wito wa kuaminiana na kujitenga na wapotoshaji.
“Uchochezi huu umeleta madhara makubwa sana, tusikubali kutumika kisiasa na wanaharakati,” ulisema ujumbe mmoja.
“Tuipende nchi yetu kwa kudumisha amani na upendo,” uliongeza mwingine.
Kama somo la vurugu hizo, wananchi wanakumbushana: “Siku moja ya vurugu ilitufundisha thamani ya miaka yote ya amani. Tuliona hasara, tukasikia vilio, lakini sasa tumejifunza. Leo tunasema: tusirudie kosa hili, tuishi kwa upendo, tujenge kwa amani.”

No comments:
Post a Comment