
Kero ya maandamano
Kufuatia matukio ya ghasia na machafuko yaliyotokea nchini kufuatia hali ya kisiasa, wananchi wengi wamejikuta katika hali ya ongezeko la msongo wa mawazo (stress) na hofu kubwa. Wataalamu wa saikolojia wanaonya kuwa kitendo hiki kimeacha makovu ya kina na kinaendelea kusababisha madhara ya kiafya ya akili kwa Watanzania, hasa wale wa kipato cha chini.
Akizungumza , Mwanasaikolojia na Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki wa Watoto (RAWATO), Peter Manyama, alieleza kuwa matukio ya vurugu yanazalisha hofu, wasiwasi, na uchungu mkubwa miongoni mwa jamii.
Akifafanua zaidi alisema:" Kuna hasara za Kimaisha: Watu wamepoteza ndugu, mali, kazi, na wengine wamejikuta kwenye deni la mikopo bila uwezo wa kulipa. Lakini pia kuna Hofu na Machungu: Maneno, picha, na kumbukumbu za vurugu zilizopita huacha historia mbaya katika akili za watu na kujenga hali ya kutoelewana hasa kwa taarifa zinazoendelea kuhusu vitisho vya kurudiwa kwa vurugu. Kama vile wito wa ‘Tarehe 9’, zinawavuruga zaidi Watanzania kwa kujiuliza, Je, kitakuwa kikubwa zaidi ya kilichopita au kidogo?"
Manyama anatahadharisha kuwa hali hii ikiachwa bila hatua za mapema, itasababisha watu wengi kuingia katika matatizo makubwa ya afya ya akili. Mmoja wa wanamitandao aliandika katika posti yake kwamba: "Mimi mpaka leo usingizi napata kwa shida sana, kila nikilala nahisi kama kuna mtu ananiamsha ."
Kataa 'Drama' Zinazonufaisha Wenye Pesa
Kutokana na maoni kutoka mtaani, kuna kilio kikubwa cha kuomba viongozi na waandaaji wa matukio ya kisiasa kuacha 'drama' hizi za maandamano, kwani zinaonekana kuwanufaisha wale wenye fedha na ajenda maalum, huku zikiwatesa na kuwarudisha nyuma wananchi wa kawaida.
"Maisha ya kweli huku mtaani ambako ndio kuna maisha halisi achana na haya maisha ya mtandaoni huku watu wamechoka na hizi drama... hizi drama ziliwarudisha nyuma watafutaji wengi ziliwapa hasara, ziliharibu muda wao wa thamani. Mtaani watu hawahitaji haya maandamano yenu."
Watu wa kipato cha chini, ambao wanategemea kazi zao za kila siku, ndio hupata hasara kubwa kunapotokea vurugu kwani ghasia hizo husimamisha biashara na shughuli za kila siku, hivyo kuwanyima walala hoi mapato ya kuendesha maisha.
Kuna madai kuwa waandamanaji wengi huandaliwa, kulipwa, na kupewa mafunzo, huku wakitamani kurubuni asilimia kubwa ya vijana wa mitaani ambao baada ya Oktiba 29 wametambua balaa la kujiingiza katika vurugu.
Hatua Zinazopaswa Kuchukuliwa
Wataalamu na wananchi wanatoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka ambapo wazazi na walezi wanatakiwa kuwajibika kikamilifu kuwalinda watoto na vijana wao dhidi ya kujiingiza kwenye vurugu au kuchochewa na wanasiasa.
Aidha Jumuiya za dini (Makanisa na Misikiti) na taasisi zingine za kijamii zinapaswa kuweka kipaumbele katika kuwajenga kisaikolojia waumini na wananchi wao ambao wameathirika na msongo wa mawazo na kupoteza mali huku wakizuia au kupunguza matamshi na vitendo vinavyoweza kuibua upya machafuko, kwa faida ya amani na ustawi wa kila Mtanzania.
No comments:
Post a Comment