Neema Nkumbi, Kahama
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, ameongoza zoezi la ugawaji wa pembejeo za kilimo kwa vijana na wanufaika 137 kutoka kata 12 za pembezoni mwa Manispaa ya Kahama, akisisitiza dhamira ya serikali ya kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mhe. Nkinda amesema serikali inatambua nafasi ya vijana katika ukuaji wa uchumi, na ndiyo sababu inaendelea kushirikiana nao ili kufikia azma ya kuhakikisha vijana wanapata uhuru wa kiuchumi kupitia kilimo chenye tija huku akiwataka wanufaika kutumia pembejeo hizo kama ilivyokusudi na kuepuka shughuli zisizo na tija.
Pembejeo hizo, zenye thamani ya shilingi milioni 70, zimegawiwa bure kwa vijana na wakulima wenye uhitaji mkubwa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Manispaa unaofadhiliwa na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Kahama.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bi. Pendo Matulanya, amesema mpango huo unalenga kuwawezesha vijana kuingia kwenye kilimo cha kisasa, sambamba na kuongeza uzalishaji katika zaidi ya ekari 370 zitakazohudumiwa na pembejeo hizo pia zitaja pembejeo hizo kuwa ni mbolea ya kupandia na kukuzia, mbegu za mahindi na alizeti pamoja na viuatilifu vya kuulia wadudu.
Baadhi ya vijana walionufaika na mpango huo, Bosco Khamis, Mohamed Juma na Winfrida Boniphace, wameshukuru serikali, wakisema kuwa hapo awali walikuwa wakilima bila mwongozo wa kitaalamu, jambo lililochangia uzalishaji hafifu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Bi. Frola Sangiwa, amesema halmashauri ina mpango wa kuongeza bajeti ili kufikia wakulima wengi zaidi, sambamba na kupunguza wimbi la vijana wan6aojihusisha na makundi na tabia zisizokubalika katika jamii.
Zoezi hilo ni mwendelezo wa mpango ulioanzishwa mwaka 2018, ambao tayari umeleta mafanikio makubwa, ikiwemo kupatikana kwa mkulima bora wa zao la pamba katika wilaya hiyo.











No comments:
Post a Comment