
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, akiwapongeza walimu wakati wakiadhimisha siku ya mwalimu duniani
Neema Nkumbi, Bukombe
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha zinapunguza upungufu wa walimu vijijini kwa kupunguza msongamano wa walimu mijini na kuwapeleka zaidi maeneo ya pembezoni.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika wilayani Bukombe mkoani Geita, Waziri Mkuu amesema serikali inaendelea kuboresha maslahi ya walimu na kusimamia sera za elimu ili kuhakikisha kila mtoto nchini anapata elimu bora.
Majaliwa amesema kuwa kwa sasa kumekuwepo na ongezeko la walimu kwa asilimia 18, ingawa bado kuna uhitaji wa walimu zaidi kutokana na wastaafu, wagonjwa na waliopoteza maisha.
Aidha, amekiri changamoto ya nyumba za walimu na kueleza kuwa serikali ipo katika mkakati wa kujenga hata magorofa ili kuhakikisha walimu wanapata makazi bora.
Katika risala ya walimu iliyosomwa na Paulo Mtenda Katibu wa chama cha walimu (CWT) Mkoa wa Geita wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule.
Paul ameelezwa kuwa kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, Mkoa wa Geita pekee umepokea zaidi ya shilingi bilioni 84.3 zilizotumika kujenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, maabara za sekondari na vyumba vya TEHAMA katika shule za msingi.
Aidha, zaidi ya walimu 823 wa shule za msingi na sekondari wamepandishwa madaraja katika mwaka wa fedha 2024/2025, hatua iliyopongezwa na walimu waliokuwa wakicheleweshwa kupanda madaraja kwa muda mrefu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Marthin Shigela, amesema "Tunamshukuru sana rais Samia kwa sababu kila analolipanga linatekelezwa, zimeletwa fedha nyingi kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya walimu na tumeshaelekezana sisi katika mkoa chini ya usimamizi wa Das kutokuendelea kutengeneza madeni ya kuhamisha walimu bila sababu za msingi".
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Caroline, amesema wizara imeendelea kuwajengea walimu uwezo kwa mafunzo ya kitaaluma, utekelezaji wa mitaala mipya na mbinu bora za upimaji ili kuinua ubora wa elimu nchini.
Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, amewapongeza walimu akisema: “Taaluma ya ualimu ndio taaluma pekee ambayo humtengeneza mtu kuwa bora Mwalimu muda wote hupambana kumfanya mtu kuwa bora kuliko yeye, hujinyima muda wake wote kumfanya mtu kuwa mume au mke bora, Mikono inayotengeneza wataalamu wote ni mikono ya mwalimu.”
Biteko amesema taaluma hii ni uumbaji wa pili kwani mara baada ya mwanadamu kuzaliwa kazi ya pili ni ya mwalimu ndiye anayetoa mwelekeo wa maisha hivyo ukiona jamii imestaarabika sababu ni mwalimu.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Walimu Wetu, Fahari Yetu.”
TAZAMA PICHA ZAIDI
No comments:
Post a Comment