VIJANA CHUO KIKUU WAONYANA UPOTOSHAJI MTANDAONI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 17 October 2025

VIJANA CHUO KIKUU WAONYANA UPOTOSHAJI MTANDAONI


Katika kipindi hiki nyeti kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo Tanzania inasherehekea demokrasia yake, tasnia ya elimu ya juu inakabiliwa na wimbi la taarifa za upotoshaji mtandaoni. Vijana na wazazi wameonywa kutoziamini taarifa zinazodai kuwa ufunguzi wa vyuo vikuu unacheleweshwa kwa sababu za kisiasa .


Wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali wamewataka wanafunzi wenzao kutopoteza muda na uvumi na badala yake kuthibitisha ratiba za masomo kupitia vyanzo rasmi vya kiserikali pekee.


TCU Yatoa Ratiba Rasmi: Ufunguzi Novemba 3



Juma Hamis, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia akili, uthibitisho na busara wanapopokea taarifa mtandaoni.


"Nashauri vijana wenzangu wajitahidi kuthibitisha taarifa kwenye vyanzo sahihi. Ukiingia kwenye tovuti au ukurasa wa Instagram wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) utakuta taarifa zote muhimu kuhusu udahili na ratiba za kufunguliwa vyuo," alisema Hamis.


Ameongeza kuwa, taarifa rasmi za TCU zilionyesha wazi kuwa dirisha la usajili lilianza tarehe 15 Julai, huku Taarifa ya Awamu ya Tatu ya Udahili iliyotolewa Oktoba 3 ikibainisha wazi kuwa vyuo vikuu vitafunguliwa rasmi tarehe 3 Novemba 2025.


"Kwa hiyo ukisikia mtu anasema eti ufunguzi wa vyuo umesogezwa kupisha uchaguzi, jiulize ana nia gani. Taarifa rasmi zipo wazi kabisa kwenye tovuti ya TCU," alisisitiza.


Kususia Habari Potofu ni Wajibu wa Uzalendo


Kwa upande wake, Janeth Shadrack, kijana kutoka Morogoro, amekemea vikali tabia ya baadhi ya vijana kuamini kila taarifa wanayoiona mtandaoni bila kujiridhisha. Alifafanua kuwa ratiba za vyuo kubadilika hutokana na mzunguko wa udahili na si kwa sababu za kisiasa, akitoa mfano wa ufunguzi wa vyuo kuahirishwa Novemba 20, 2020, kutokana na janga la Corona, na si Uchaguzi Mkuu uliokuwepo wakati huo.


"Ni lazima tujifunze kuchuja taarifa. Si kila kinachoandikwa ni kweli," alisisitiza Janeth.


Alipinga vikali madai kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amezuia vyuo vikuu kufunguliwa, akisisitiza kuwa taarifa hizo ni za upotoshaji na hazina msingi wowote. "Serikali inaendelea kuhakikisha elimu inatolewa kwa wakati na kwamba wanafunzi wote wanapata haki yao ya msingi bila usumbufu wowote," alisema Janeth, akionya kuwa vijana wasitumiwe kueneza uchochezi.


Kwa mujibu wa taarifa ya TCU, kuongeza Awamu ya Tatu ya Udahili ni hatua ya kutoa nafasi kwa waombaji ambao hawakupata vyuo katika awamu zilizopita, pamoja na wale waliodahiliwa katika vyuo zaidi ya kimoja kuthibitisha rasmi chuo wanachotaka kuhudhuria.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso