NSSF MKOA WA KAHAMA YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KWA KUTAMBUA MICHANGO YA WATEJA WAKE - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 10 October 2025

NSSF MKOA WA KAHAMA YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KWA KUTAMBUA MICHANGO YA WATEJA WAKE



Kahama. 

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Kahama umeadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kutambua mchango mkubwa wa wateja wake, katika hafla iliyofanyika leo oktoba 10, 2025, katika viunga vya ofisi za mfuko huo.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Meneja wa NSSF Mkoa wa Kahama, Bi. Aisha Nyemba, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuimarisha uhusiano kati ya NSSF na wateja wake pamoja na kutambua mchango wao unaoendelea kuufanya mfuko huo kuwa imara.


“Tumeungana na wateja wetu kutambua mchango wao, maana wao ndio wanaotufanya tuendelee kuonekana, Wiki hii tumeiboresha kwa kuongeza viburudisho, lakini huduma zetu zimeendelea kama kawaida kwa kuwa NSSF inalenga kutoa huduma bora kila siku,” amesema Bi. Nyemba.

Ameongeza kuwa, kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Kidigitali Tumeweza”, ambayo imeonyesha mafanikio makubwa katika matumizi ya mifumo ya kidigitali ndani ya NSSF.


“Wateja wetu sasa wanaweza kujisajili, kuandikisha wanachama wapya, kufungua madai, na kufuatilia michango yao kupitia mfumo wa kidigitali wakiwa popote walipo,” ameongeza.

Bi. Nyemba pia amebainisha kuwa NSSF mkoa wa Kahama ina dawati maalum la kuwasaidia wateja ambao wanapata changamoto katika kutumia mifumo ya kidigitali, ili kuhakikisha kila mwanachama anapata huduma bila usumbufu.

Kwa upande wake, Bi. Bertha Mwambe, Ofisa Mwandamizi wa Mafao NSSF Kahama, amesema wameboresha huduma za online ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama.


“Tumeweka dawati la kuwasaidia wanachama wanaofungua madai online. Tunawaelekeza hatua kwa hatua hadi mwajiri anapopitisha maombi yao. Mfumo huu umefanya huduma kuwa rahisi na za haraka,” amesema Bi. Mwambe.

Rehema Wilson, mkazi wa Mwime na mjasiriamali, ametoa shukrani kwa NSSF kwa huduma bora wanazozitoa, akisema sasa ana uhakika wa huduma za afya kupitia bima anayopata kama mwanachama wa NSSF.


“Tunashukuru kwa huduma nzuri. Si kwa wiki hii tu, bali hata siku za kawaida huduma ni bora. Kupitia NSSF sasa nina uhakika wa afya yangu na familia yangu,” amesema Rehema.

Naye Monica Lazaro Mange, mjasiriamali kutoka Igomelo, amesema NSSF imempa uhakika wa maisha kutokana na mafao ya afya na pensheni anayotarajia kuyapata baada ya kuchangia kwa miaka 15.


“Kikubwa ni elimu maana Watu wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu manufaa ya NSSF, Mimi binafsi ninaona hakuna tofauti kati yangu na mfanyakazi wa Serikali,” amesema Monica.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kimataifa kila mwezi Oktoba, Kwa mwaka 2025, maadhimisho hayo yamefanyika kuanzia tarehe 6 hadi 10 Oktoba yakibebwa na kaulimbiu ya kimataifa isemayo “Mission Possible”, huku NSSF ikiadhimisha chini ya kaulimbiu ya kitaifa “Kidigitali Tumeweza.”


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso