
Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwandani Kata ya Mjini Manispaa ya Shinyanga Ashraf Majaliwa akizungumzia tukio hilo.

Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Viwandani Manispaa ya Shinyanga wakiwa eneo la tukio
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
***
Katika tukio la kusikitisha, mwili wa mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi minane umekutwa ndani ya mfuko wa taka nje ya hosteli ya wanafunzi katika Mtaa wa Viwandani, Manispaa ya Shinyanga, hali iliyosababisha taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.
Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo limebainika baada ya mkazi wa eneo hilo, Jeremia Evansi, alipokuwa akitafuta mabaki ya vyakula kwenye mifuko ya taka kwa ajili ya kulisha kuku, ndipo alipogundua mwili wa mtoto huyo.
“Wakati napitapita katika mifuko nikitafuta chakula cha kuku, nikakuta mfuko wenye taka. Nilipofungua, nikashangaa kuona kichanga ndani yake. Mimi huwa natafuta mabaki ya vyakula kwa ajili ya kuku wangu wanaopatikana soko la Nguzo Nane,” amesema Evansi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwandani, Ashraf Majaliwa, amelaani tukio hilo akilieleza kuwa ni kitendo cha ukatili wa hali ya juu na ukiukaji wa haki za binadamu.
“Ni jambo la kusikitisha sana. Tunatoa wito kwa wanawake na mabinti kuepuka vitendo vya namna hii ambavyo ni kinyume cha sheria na utu wa binadamu,” amesema Majaliwa.
Ameeleza kuwa baada ya kugundulika, mwili wa mtoto huyo ulitolewa kwenye mfuko wa taka na kuwekwa kwenye boski, kisha polisi walifika na kuuchukua kwa uchunguzi zaidi.
Jeshi la Polisi limefika eneo la tukio na kuuchukua mwili huo kwa ajili ya uchunguzi wa kina ili kubaini mhusika aliyefanya ukatili huo wa kutisha.
WITO KWA JAMII
Tukio hili linaibua swali kubwa kuhusu mmomonyoko wa maadili na thamani ya uhai wa binadamu. Jamii inahimizwa kuendelea kulinda haki na usalama wa watoto, na mtu yeyote anayepata taarifa au dalili za vitendo vya ukatili au utelekezaji awasilishe taarifa hizo haraka kwa vyombo vya dola au viongozi wa mtaa.
Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na ni jukumu la kila mmoja kulinda maisha yao tangu wakiwa tumboni hadi wanapokua.


Jeremia Evansi mkazi wa Matanda ambaye alibaini uwepo wa mwili wa mtoto mchanga kwenye mfuko wa taka wakati akitafuta mabaki ya vyakula kwa ajili ya kuku.


Wananchi wakiwa eneo la tukio

No comments:
Post a Comment