
Na Neema Nkumbi, Kahama
Mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 3 hadi 4 amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa kipigo na bibi yake, Christina Kishiwa, ambaye ni mama mdogo wa mama yake mzazi, katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa marehemu alishambuliwa kwa fimbo na bomba la plastiki baada ya kudaiwa kutomsalimia bibi yake asubuhi na jioni, pamoja na kujikojolea.
MAELEZO YA FAMILIA
Mwanafamilia mmoja (jina limehifadhiwa) amesema awali walipewa taarifa kuwa mtoto ameteleza ndani na kufariki dunia, na waliombwa kujiandaa kwa mazishi ya haraka.
“Nilipoona alama za fimbo mwilini mwa mtoto ndipo nilipomhoji Mama yake hakusema chochote hadi nilipoita polisi, ndipo akaeleza kuwa mtoto alipigwa na mama Kennedy (mtuhumiwa), ambaye alitaka mtoto azikwe haraka bila familia kufahamu ukweli,” amesema.
KAULI YA UONGOZI WA MTAA
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato, Kata ya Nyasubi, Hussein Mwita, ameeleza kuwa alipokea taarifa saa 3 usiku kupitia wasamaria wema kuhusu tukio hilo.
“Nilipofika eneo la tukio, polisi walikuwa tayari wamefika na kuchukua mwili wa mtoto na mama yake, Mama mwenye nyumba alikuwa ameshaondoka na kutokomea kusikojulikana, Niliwahi kusikia historia yake kuwa aliwahi kumchoma mfanyakazi wa ndani kwa pasi, hivyo kitendo hiki si cha kwanza kwake,” amesema.
MASHUHUDA
Jenifa Emanuel, mpangaji wa mtuhumiwa, amesema alishtushwa baada ya mama mzazi wa marehemu kumwambia mtoto wake amefariki kwa kupigwa na mama mwenye nyumba.
Bakari Hamis, shuhuda mwingine, amesema walipokea taarifa kuwa mtoto ameanguka, lakini walipofika eneo la tukio walibaini kuwa alikuwa amepigwa, hivyo kutoa taarifa polisi.
TAARIFA YA HOSPITALI
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Michael Mushi, amesema walipokea mwili wa mtoto saa 4 usiku na uchunguzi wa awali ulionesha alikuwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani, tumboni, kifuani, mgongoni, mikononi na miguuni.
JESHI LA POLISI
Kamanda Magomi amelaani vikali vitendo vya ukatili vinavyofanywa na baadhi ya watu na kusema jitihada za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea.
No comments:
Post a Comment