Mkuu wa Mkoa Mboni Mhita Apongeza Utulivu na Mwitikio Mkubwa wa Wananchi Kupiga Kura
Na Neema Nkumbi Kahama
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema kuwa hali ya uchaguzi katika mkoa huo ni shwari na wananchi wamejitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura kwa amani na utulivu.
Akizungumza leo baada ya kupigia kura katika kituo cha kata ya Igalilimi Manispaa ya Kahama, Mhita amesema kuwa wananchi wameonyesha mwitikio chanya na nidhamu ya hali ya juu katika kushiriki zoezi hilo muhimu la kidemokrasia.
“Nimefarijika kuona wananchi wetu wakipiga kura kwa amani na kutimiza haki yao ya kikatiba, Mkoa uko shwari, vituo vya kupigia kura vipo vya kutosha, na wananchi wanapokelewa kwa wakati,” amesema Mkuu wa Mkoa.
Mhita ameongeza kuwa hadi sasa hakuna taarifa zozote za vurugu au viashiria vya uvunjifu wa amani katika kata zote 130 za mkoa wa Shinyanga pia ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea kudumisha upendo, amani na utulivu wakati na baada ya uchaguzi.
“Tupende nchi yetu, tuendelee kuilinda amani tuliyonayo, na tuhamasishane kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa kidemokrasia,” amesisitiza.
Mhita ameambatana na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, Katibu Tawala wa Wilaya, Glory Absolomon, na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, pamoja na watumishi wengine wa serikali katika kupiga kura.







No comments:
Post a Comment