MKANDARASI KAHAMA KUKATWA SHILINGI MILIONI 2 KILA SIKU KWA KUKIUKA MKATABA WA UJENZI WA BARABARA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 2 October 2025

MKANDARASI KAHAMA KUKATWA SHILINGI MILIONI 2 KILA SIKU KWA KUKIUKA MKATABA WA UJENZI WA BARABARA



Na: Neema Nkumbi, Kahama 

Serikali mkoani Shinyanga imeanza kumchukulia hatua mkandarasi Sichuan Road & Bridge Co Ltd, anayetekeleza ujenzi wa barabara na mifereji ya maji ya mvua katika Manispaa ya Kahama, baada ya kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati kinyume na makubaliano ya mkataba.

Mradi huo una thamani ya zaidi ya Sh20.864 bilioni na ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi 15 kuanzia Novemba 20, 2023 hadi Februari 2025. Hata hivyo, baada ya kupewa nyongeza ya muda hadi Mei 19, 2025, na kisha hadi Septemba 30, 2025, bado mradi huo haujakamilika.

SERIKALI YACHUKUA HATUA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameelekeza mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, kuandika barua rasmi kwa mkandarasi huyo kuanza kukatwa Sh2 milioni kila siku kuanzia Oktoba 1, 2025 kwa mujibu wa mkataba.

Mhita amesema serikali haitatoa muda mwingine wa nyongeza na kuongeza kuwa hatua za kisheria zinaendelea kuandaliwa na wanasheria wa Halmashauri.


“Hawa wenzetu wamekuwa wajanja, kila siku wanaomba nyongeza ya muda. Hatutakubali. Kuanzia leo tunaanza kuwatoza Sh2 milioni kila siku kwa mujibu wa mkataba,” amesema.

MKANDARASI AJITETEA

Mkandarasi Sichuan Road & Bridge Co Ltd ameomba kuongezewa muda akidai changamoto kubwa ni uwepo wa maji ya ardhini karibu na eneo la mradi.
Mhandisi mshauri wa mradi, Samwel Mtawa, amesema ujenzi wa barabara upo hatua ya umwagaji lami na kwa mashine walizonazo, wana uwezo wa kumaliza ndani ya siku 45–60 endapo hali ya hewa itaruhusu.
MAONI YA WANANCHI

Wananchi wa maeneo yanayopitiwa na barabara hizo wameilalamikia kampuni hiyo kwa kuchelewesha mradi na kuwaletea kero.


John Mathayo, mkazi wa Majengo:

“Miundombinu ya sasa ni kero kubwa na tunaelekea kipindi cha mvua, mvua ikianza kunyesha maji yanajaa kwenye nyumba zetu, na tunakosa  sehemu ya kupita, mkandarasi amalize mapema kabla ya mvua.”


Maisha Masanyiwa, mfanyabiashara wa Nyasubi:


“Tumefunga maduka kwa zaidi ya miezi mitatu bila biashara, lakini bado tunadaiwa kodi na mikopo, Mkandarasi amalize haraka ili tuweze kuendelea na kazi.”
HATUA ZA SERIKALI KUU

Mnamo Machi 18, 2025, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Zainab Katimba, alionya kuwa iwapo mkandarasi huyo atashindwa kukamilisha kazi kwa wakati, serikali itavunja mkataba na atapoteza sifa ya kupewa kazi nyingine nchini.
MAELEZO YA MRADI

Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Kupendezesha Miji (TACTIC) unaotekelezwa katika Halmashauri 45 nchini. Katika Manispaa ya Kahama unahusisha:
Ujenzi wa barabara kuu za mjini (Km 12.03)
Barabara za eneo la viwanda Zongomela (Km 3.06)
Ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua maeneo ya Chelsea–Lyazungu na Shunu–Magobeko (Km 4.9)


MWISHO

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso