KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI ATAKA VYANZO VIDOGO VYA MAJI VITUNZWE - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 17 September 2025

KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI ATAKA VYANZO VIDOGO VYA MAJI VITUNZWE

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri akizungumza na waandishi mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa chujio la maji Kahama

Na Neema Nkumbi, Kahama

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amezitaka mamlaka za maji nchini kuhakikisha zinatunza na kuendeleza vyanzo vidogovidogo vya maji ili viwe mbadala wakati miradi mikubwa inapokuwa inafanyiwa marekebisho.

Mhandisi Mwajuma ametoa wito huo septemba 16, 2025 alipotembelea mradi wa ujenzi wa chujio la maji Mwendakulima, Manispaa ya Kahama, lenye uwezo wa kuchuja lita milioni 10 kwa siku.


“Tuna vyanzo vya zamani kama mabwawa na visima ambavyo bado ni muhimu, Mamlaka hazipaswi kuviacha kwa sababu tu miradi mikubwa ipo, Pale mradi mkubwa unapohitaji marekebisho, wananchi watabaki bila huduma iwapo hatutavitunza hivi vyanzo vya zamani,” amesema.

Aidha, ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa chujio hilo, akibainisha kuwa usanifu wake umefanywa na wataalamu wa ndani kwa kushirikiana kati ya Mamlaka ya Maji Kahama na taasisi nyingine za maji.


“Nimefurahishwa sana kuona mradi huu mkubwa unasimamiwa na wataalamu wetu wa ndani Pia mkandarasi anayetekeleza ni wa ndani, jambo linaloonesha serikali inatekeleza dhana ya kujenga uwezo wa wazawa,” ameongeza.

Vilevile, Katibu Mkuu amewataka wahandisi wa ndani kutumia fursa zinazotolewa na serikali ili kujijengea uzoefu utakaowapa ujasiri katika utekelezaji wa miradi mikubwa ijayo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama, Bw. Allen Marwa 


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama, Bw. Allen Marwa, amesema mradi huo unalenga kuhakikisha wananchi hawakosi huduma hata pale inapojitokeza dharura kwenye miradi mikubwa.

Marwa ameongeza kuwa mamlaka yake imejipanga kukamilisha mradi huo ifikapo Februari 2026, kwa mujibu wa muda uliopangwa.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso