
Na Neema Nkumbi, Kahama
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ushetu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Cherehani, amemnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, kwa wananchi wa jimbo hilo.
Cherehani amemnadi Ngayiwa katika uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika Jumapili Septemba 14,2025 eneo la Phantom, Kata ya Nyasubi, Manispaa ya Kahama.
Tukio hilo la kumnadi Ngayiwa limepewa baraka na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, ambaye amempa ridhaa Cherehani kufanya utambulisho huo na kumnadi kwa kuwa yeye ni mbunge mwenyeji wa wilaya hiyo katika nafasi ya ubunge.
Akizungumza mbele ya wananchi waliojitokeza kwa wingi, Cherehani amewasihi wakazi wa Kahama kumpa kura Ngayiwa katika uchaguzi mkuu ujao huku akisisitiza kuwa Ngayiwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kuwasemea wananchi bungeni na kushughulikia changamoto za msingi ikiwemo maji, ujenzi wa miundombinu, na huduma za kijamii.
“Mahitaji ya wana Kahama ninayafahamu, na naamini Ngayiwa ataweza kuyasimamia vizuri bungeni ili maendeleo yaende kwa kasi hivyo mchagueni Ngayiwa,” amesema Cherehani.
Kwa upande wake, Ngayiwa amenadi ilani ya Chama Cha Mapinduzi huku akiwaomba wananchi kumchagua Rais samia madiwani na yeye pia ili kuleta maendeleo zaidi kwa wananchi
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amewataka wananchi kuhakikisha wanawachagua wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge hadi Udiwani, ili kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo.

No comments:
Post a Comment