WANANCHI WA NYAHANGA WAILALAMIKIA KUWASA JUU YA UPOTEVU WA MAJI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 21 August 2025

WANANCHI WA NYAHANGA WAILALAMIKIA KUWASA JUU YA UPOTEVU WA MAJI


NA NEEMA NKUMBI-HUHESO DIGITAL KAHAMA

Wananchi wa mtaa wa Shunu, kata ya Nyahanga, Manispaa ya Kahama wameeleza kero zao kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Mkinda, wakidai Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) kushindwa kushughulikia mivujo ya maji kwa wakati, hali inayopelekea hasara kubwa na bili zisizoendana na matumizi yao.

Mmoja wa wananchi hao Daniel Msana amesema mabomba yakipasuka huchukua hata miezi miwili bila kurekebishwa licha ya kutoa taarifa, na kuhoji iwapo maji yanayopotea huongezwa kwenye bili za wateja.

Akijibu malalamiko hayo, Afisa Mahusiano wa KUWASA, John Mkama, amekiri kuwepo kwa mivujo katika maeneo mbalimbali, akibainisha kuwa baadhi hujitokeza kwenye vichochoro hali inayofanya isiwe rahisi kugundulika mapema.
“Tumeweka utaratibu wa kushirikiana na wananchi ili kuibaini mivujo hiyo, Tuna simu za bure 0800110320 na 0800110321 kwa ajili ya kutoa taarifa, Hili lililotolewa na mwananchi tumelipokea na tutalifanyia kazi,” amesema.

Katika hatua nyingine, mkazi wa Shunu Hongwa, Mzee Mwita, amelalamikia ukosefu wa maji ya bomba akisema maji wanayotumia hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Akitoa ufafanuzi, Mkama amesema: “Ni kweli eneo la Hongwa linachangamoto za kitaalamu,Tulibaini miundombinu iliyolazwa haikuwa na ubora unaotakiwa,Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kubadilisha mabomba na kuanzia kesho mradi huo unakamilika ili wananchi waanze kupata huduma bora.”

Aidha, mkazi wa mtaa wa Mtakuja, Steven Joseph, amesema mradi wa ujenzi wa tanki la maji ulioanzishwa na KUWASA umekwama licha ya kuahidiwa na mamlaka hiyo wakati wa mkutano na Mkuu wa Mkoa kuwa watakamilisha ndani ya mwezi mmoja.

Kuhusu hilo, Mkama amethibitisha kuwa mradi huo wenye thamani ya Shilingi milioni 442 umekamilisha awamu ya kwanza ya ulazaji mabomba kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 257, huku ujenzi wa tanki ukiwa umesimama kwa kufikia asilimia 47 baada ya mkandarasi kutopewa malipo ya vyeti vyake.
“Tunafahamu changamoto ya wananchi wa Mtakuja. Mazungumzo ya kuhakikisha mkandarasi analipwa yanaendelea, ili akamilishe tanki litakalowahudumia wananchi wote wa eneo hilo ikiwemo Shule ya Sekondari Nyahanga, Kwa sasa tumeunganisha maji moja kwa moja shuleni ili wanafunzi angalau waanze kupata huduma wakati tukisubiri kukamilisha kazi,” ameeleza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Mkinda, amewashukuru wakazi wa Nyahanga kwa kuwa wawazi na kutoa kero zao, Hata hivyo amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa na watendaji kutimiza wajibu wao.


“Changamoto hizi nyingi mnazifahamu. Kama mngetengeneza mazingira mazuri ya kufanya mikutano mngeweza kutatua changamoto mlizo na uwezo nazo, na zilizowashinda mngezipeleka kwenye idara husika. Ninyi ndio injini ya shughuli zote tunazofanya wilayani, sikilizeni wananchi na pale mnapokwama tushirikiane tutatue changamoto, pia KUWASA hakikisheni mnatatua malalamiko yaliyotolewa,” amesema Mkinda.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso