WAANDISHI NA WATANGAZAJI WA KANDA YA ZIWA WAPEWA MAFUNZO YA MWONGOZO WA KURIPOTI UCHAGUZI MKUU 2025 - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 7 August 2025

WAANDISHI NA WATANGAZAJI WA KANDA YA ZIWA WAPEWA MAFUNZO YA MWONGOZO WA KURIPOTI UCHAGUZI MKUU 2025


Mhandisi Andrew Kisaka kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) akiwasilisha mada kuhusu Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa za mwaka 2020 na namna bora ya kuripoti migogoro na majanga wakati wa uchaguzi


Na Neema Nkumbi – Huheso Digital, Mwanza


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imeendesha semina kwa waandishi wa habari na watangazaji wa Kanda ya Ziwa, ikiwa ni maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Semina hiyo imefanyika leo Agosti 7, 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania jijini Mwanza, ikihusisha zaidi ya washiriki 100 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Mara na Kagera.


MADA SABA ZA MSINGI ZAWASILISHWA


Katika semina hiyo, mada saba zimewasilishwa zilizolenga kukuza weledi, uelewa wa majukumu yao, na kuimarisha ushirikiano baina ya vyombo vya habari na wadau wa uchaguzi.


1. Uandishi wa Habari za Uchaguzi


Mada ya kwanza imewasilishwa na Dkt Egbert Mkoko kutoka Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), ambapo wanahabari wameelimishwa kuhusu kanuni za kitaaluma, usawa kwa vyama vya siasa, ukamilifu wa taarifa, na namna ya kulinda mshikamano wa kitaifa.


2. Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi


Mada hii imewasilishwa na Mhandisi Andrew Kisaka kutoka TCRA, kanuni za mwaka 2020 kuhusu matangazo ya vyama vya siasa, ikisisitiza uwiano wa muda wa matangazo, usimamizi wa maudhui ya kampeni, na wajibu wa watoa huduma kuhakikisha uadilifu na uwazi.


3. Usalama na Ushirikiano na Vyombo vya Dola


Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, DCP David Misime, ameeleza wajibu wa wanahabari katika kulinda usalama wakati wa uchaguzi, Amehimiza ushirikiano kati ya waandishi na vyombo vya usalama ili kuhakikisha taarifa zinatolewa kwa njia salama na ya kisheria.


4. Maadili na Sheria za Uandishi


JAB iliwasilisha mada kuhusu maadili na sheria zinazowaongoza wanahabari, ikisisitiza kuepuka uchochezi, uvunjaji wa sheria, na kuzingatia haki za watu wanaotajwa katika habari.


5. Mitandao ya Kijamii na Akili Bandia (AI)


Wataalamu wa SJMC waliwasilisha namna mitandao ya kijamii na teknolojia ya AI inavyoathiri mwenendo wa uchaguzi. Waandishi walihimizwa kuwa makini na taarifa potofu na kuhakikisha uthibitisho kabla ya kuchapisha.


6. Kuripoti Migogoro na Majanga
Mhandisi Andrew Kisaka kutoka  TCRA pia ilitoa mwongozo wa kuripoti migogoro kwa weledi, kwa kutumia lugha ya staha na kuepuka taarifa zinazoleta hofu au chuki katika jamii.


7. Ulinzi wa Taarifa Binafsi


Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, kupitia Mkuu wa Mawasiliano Serikalini Innocent Mungy, ilisisitiza umuhimu wa kulinda taarifa za watu binafsi wakati wa uchaguzi, hususan katika ukusanyaji na uchakataji wa taarifa.


Aidha, semina hiyo imeangazia nafasi ya teknolojia ya kisasa katika kuendesha na kuripoti uchaguzi, ikiwa ni hatua muhimu katika kuandaa vyombo vya habari kwa majukumu yao kwenye zama za kidijitali.
Dkt Egbert Mkoko kutoka Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC)
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini DCP David Misime, akiwasilisha mada kuhusu wajibu wa wanahabari na vyombo vya dola katika kulinda usalama kipindi cha uchaguzi.
Wakili Rehema kutoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) akiwasilisha mada kuhusu maadili na sheria zinazowaongoza waandishi wa habari nchini
Mtaalamu wa maudhui ya utangazaji na habari Dkt Darius Mukiza kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), akiwasilisha mada kuhusu Mitandao ya Kijamii na Akili Bandia (AI) kuelekea Uchaguzi

PICHA: Na Kadama Malunde








No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso