VYOMBO VYA HABARI NA POLISI WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUIMARISHA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 7 August 2025

VYOMBO VYA HABARI NA POLISI WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUIMARISHA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI

 


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa waandishi wa habari na watangazaji kutoka Kanda ya Ziwa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha taarifa zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinaripotiwa kwa weledi, usahihi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.


Na Neema Nkumbi, Huheso Digital – Mwanza


Katika kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unafanyika kwa amani na utulivu, vyombo vya habari na Jeshi la Polisi wametakiwa kushirikiana kwa karibu zaidi, kubadilishana taarifa na kulinda maslahi ya taifa.


Wito huo umetolewa leo Agosti 7, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, wakati wa kufunga Semina ya Waandishi wa Habari na Jeshi la Polisi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, iliyolenga kuwajengea uwezo kuelekea uchaguzi huo mkubwa.


“Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kudhibiti taarifa potofu, lakini vinahitaji kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha amani inadumu wakati huu nyeti,” amesema Mtanda.


Mtanda ameongeza kuwa kwa kufanya kazi kwa ukaribu, vyombo hivyo viwili vinaweza kusaidia kuzuia taharuki, kuchochea mijadala ya kitaifa yenye staha, na kuwalinda wananchi dhidi ya taarifa zisizo sahihi.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Rodney Mbuya, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka, yakilenga si tu kuwajengea uelewa waandishi wa habari juu ya sheria na maadili, bali pia kuimarisha mahusiano yao na polisi.


“Jeshi la Polisi linatakiwa kuwalinda waandishi wa habari, hasa kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi, ili waweze kutekeleza majukumu yao bila vitisho wala hofu,” amesema Mbuya.


Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika semina hiyo ni pamoja na mwongozo wa kuripoti uchaguzi, wajibu wa vyombo vya habari na Jeshi la Polisi, matumizi ya akili bandia katika habari, ulinzi wa taarifa binafsi, na usimamizi wa maudhui yenye uwezekano wa kuchochea migogoro.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso