Neema Nkumbi – Huheso Digital, Kahama
Tukio la kuuawa kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Busalala, kata ya Mwendakulima katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, limezua hofu kwa walimu na wakazi wa eneo hilo, huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi kubaini chanzo na wahusika wa tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi, amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Agosti 9, 2025, ambapo marehemu Fatuma Khamis alikutwa amekatwa shingo na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana. Amesema uchunguzi wa awali umebaini kulikuwepo na mgogoro wa kifamilia, na kwa sasa wanamshikilia mume wa marehemu kwa mahojiano zaidi.
“Upelelezi unaendelea ili kubaini kiini cha tukio hili, Tunatoa wito kwa familia kutatua migogoro yao kwa amani na kuachana na vitendo vya ukatili,” amesema Magomi.
Mwenyekiti wa Nzengo ya Budushi, Richard Charles, amesema tukio hili ni la tatu la aina hiyo katika eneo lake ndani ya kipindi kifupi, na kwamba wananchi wameanza kuchukua tahadhari kwa kuweka mfumo wa kuwasiliana haraka endapo kutatokea tukio la dharura.
“Tumeshaona wanaume na wanawake wakishambuliwa kwa mapanga na kuuawa na watu wasiojulikana, Sasa tunahimiza kila jirani awe na mawasiliano ya jirani yake,” amesema Charles.
Jirani wa marehemu, Gervas Gabriel, amesema kifo hicho kimewaacha na simanzi kubwa, akimtaja marehemu kama mtu mwenye ushirikiano na upendo, Wakati huo huo, mwalimu mwenzake, Rachel Isaac, amesema tukio hilo limeongeza hofu miongoni mwa walimu na kuomba serikali kuongeza ulinzi na kuimarisha usalama kwa watumishi wa elimu.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mtoto wa marehemu mwenye umri wa miaka minne ndiye aliyegundua mwili wa mama yake ukiwa umelala chini na damu nyingi, na kutoa taarifa kwa majirani.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment