Mkurugenzi Mtendaji wa 101 Group, Gideon Kabakeza akizungumza na waandishi wa habari juu ya ukaribisho wa maadhimisho ya miaka 4 ya The magic 101
Na Neema Nkumbi – Huheso Digital, Kahama
Mkurugenzi Mtendaji wa 101 Group, Gideon Kabakeza, ameishukuru jamii kwa ushirikiano walioutoa katika kipindi cha miaka minne ya kampuni hiyo, akisisitiza dhamira yao ya kuendelea kurudisha shukrani kwa vitendo.
Akizungumza na waandishi wa habari agosti 9,2025 katika ukumbi wa mikutano wa The Levels 101, Kabakeza amesema kilele cha maadhimisho ya miaka minne ya The Magic 101 kitafanyika Agosti 23, 2025 na kupambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo Mbosso Khan.
Ameeleza kuwa kama sehemu ya kusherehekea na kuonyesha mshikamano na jamii, kampuni hiyo imejipanga kuchangia shilingi 200,000 kila mwezi kutoka sehemu ya faida wanayopata, kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali kujikwamua kiuchumi.
“Katika miaka minne tumefanikisha mambo mengi ya kijamii, ikiwemo kugharamia bili za wagonjwa hospitalini, kusaidia vituo vya watoto yatima na kuchangia mahitaji mbalimbali. Tunajivunia kuendelea na utamaduni huu katika maadhimisho yetu ya mwaka huu,” amesema Kabakeza.
The Magic 101 Group imefungua fursa za ajira kwa vijana zaidi ya 200, wakiwemo wenye taaluma na wasio na taaluma, sambamba na kutoa huduma za burudani na chakula. Kwa sasa, kundi hilo linaundwa na kampuni nne: The Magic 101, The Levels 101 Hotel, Migahawa ya 101 iliyopo Tanzania na China, pamoja na Logistics 101 Group.
Kabakeza pia ameishukuru serikali kwa ushirikiano inaoutoa na kuiomba jamii kuendelea kuwaunga mkono. Amewakaribisha wakazi wa Kahama na maeneo jirani kuhudhuria sherehe za kilele cha maadhimisho hayo.
No comments:
Post a Comment