Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Adam Mihayo akizungumza na wadau wa benki ya TCB
Na Neema Nkumbi, Huheso Digital Kahama
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Adam Mihayo, amesema kuwa benki hiyo inaweza kumkopesha mteja mmoja zaidi ya Shilingi Bilioni 35, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuiwezesha sekta binafsi na wateja wake kuinuka kiuchumi.
Amesema hayo Agost 8,2025 katika usiku uliokutanisha wadau kwa chakula cha usiku (Dinner Gala) iliyofanyika wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, iliyoandaliwa na TCB kwa lengo la kukutana na wateja na wadau wake, pamoja na kuwashukuru kwa kuendelea kuamini huduma za benki hiyo, Tukio hilo pia lilihusisha maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo.
Mihayo amebainisha kuwa mwaka jana benki hiyo ilipata faida ya Shilingi Bilioni 44 kabla ya kodi, akieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na kuwa na wateja wazuri na waaminifu ambao wanakopa na kurejesha mikopo kwa wakati.
“Kahama pia ni sehemu tunayoitazama kimkakati kutokana na fursa mbalimbali zilizopo, ikiwemo sekta ya kilimo, madini na biashara,” amesema Mihayo.
Ameongeza kuwa kutokana na zao la tumbaku kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati katika eneo hilo, TCB imeweza kutoa takribani Shilingi Bilioni 10 kwa wakulima wa tumbaku ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji na kipato.
Aidha, amefafanua kuwa benki hiyo inahudumia kwa karibu wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa kutoa mikopo hadi Shilingi Milioni 70 kwa dhamana ndogo tu ambapo mwaka jana TCB ilitoa jumla ya mikopo zaidi ya Shilingi Bilioni 360 kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, akisisitiza kuwa kundi hili ni muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha, amesisitiza kuwa ili benki iweze kuwa na ushindani na mabenki mengine, ni lazima ijenge uwezo wa kutoa huduma kwa wateja wa aina na viwango mbalimbali, kuanzia wateja binafsi, wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.
Mihayo amekumbusha pia kuwa TCB inamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 87, akibainisha kuwa benki hiyo ni mali ya wananchi wote kwani serikali imewekeza kupitia kodi wanazolipa. “Hii ni benki yenu, tuitumie kwa manufaa ya maendeleo ya taifa letu,” ameongeza.
Amesema benki inaamini kuwa ikiwasaidia wateja kukua kibiashara, wataweza kuunda ajira nyingi na kupanua wigo wa serikali katika kukusanya kodi, jambo litakaloongeza mapato ya taifa na kuchochea maendeleo pia wataepukana na mikopo yenye matatizo (mikopo umiza).
“Tunawaahidi wana Kahama kwamba tuko vizuri, tumejipanga, tuna ukwasi wa kutosha na tuko tayari kuwahudumia kwa huduma za kisasa, salama na za uhakika,” amesisitiza.
Mmoja wa wadau wa TCB, Asha Hussein, mjasiriamali wa ufugaji wa kuku wa mayai, amesema benki hiyo imewasaidia kwa kutoa semina mbalimbali na mikopo ambayo imemuwezesha kuhamia katika ufugaji wa kuku badala ya kuishi na kuku tu.
“Katika sekta ya kilimo tulikuwa tunachukuliwa kawaida, lakini kupitia TCB, wakulima tunafanya vizuri,” amesema Asha.
Kwa mujibu wa taarifa ya benki hiyo, maadhimisho ya miaka 100 yanalenga kuonyesha mchango wa TCB katika kujenga uchumi wa taifa kupitia utoaji wa huduma bora, ubunifu wa bidhaa mpya na kuimarisha uhusiano na wateja wake kote nchini.
No comments:
Post a Comment