TAHARUKI KAHAMA: JENEZA LATUPWA SHIMONI, WANANCHI WABAKI NA MASWALI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 13 August 2025

TAHARUKI KAHAMA: JENEZA LATUPWA SHIMONI, WANANCHI WABAKI NA MASWALI



Na Neema Nkumbi, Huheso Digital – Kahama

Wananchi wa eneo la Nyamela Izuga, Mtaa wa Mhongolo, Manispaa ya Kahama, wamepigwa na butwaa baada ya kukuta jeneza lililotumika limetelekezwa kwenye shimo la kuchimba mchanga (mworamu).

Mwenyekiti wa mtaa huo, Emanuel Nangale, amesema tukio hilo lilitokea Jumamosi na liligunduliwa na wananchi waliokuwa wakipita karibu na shimo hilo, kisha kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali ya mtaa.

“Tulifika eneo la tukio na kukuta jeneza hilo likiwa na kamba za kushushia kaburini, udongo na alama za damu. Ndani yake kulikuwa na viashiria vilivyoonyesha kuwa liliwahi kuwa na mwili,” amesema Nangale.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Hadija Salum, amesema siku hiyo walikuwa katika msiba wa jirani yao, Nzengo, na walipata taharuki kubwa kwani tukio kama hilo halijawahi kutokea katika mtaa huo.

“Tulipolifikia jeneza tulilikagua na kukuta nguo kama suruali, sanda na koti, Hali hiyo ilitupa hofu kubwa na baadhi ya watu kuhusisha tukio hilo na imani potofu za kishirikina,” ameeleza.

Shuhuda mwingine, Sharifu Said, amesema huenda jeneza hilo lilifukuliwa eneo tofauti na kuletwa hapo, kwa kuwa walipotembelea makaburi ya mtaa huo hawakuona dalili za kaburi lililofukuliwa.
“Labda itakuwa ni kazi za waganga wa kienyeji na ushirikina, Binafsi limenichanganya sana, ila nawashauri wananchi wenzangu kuendelea kupeana taarifa zaidi na kufikisha kwa viongozi wetu,” amesema.

Viongozi wa mtaa walijaribu kufanya ufuatiliaji kwa wananchi na kutembelea maeneo ya makaburi ili kubaini kama kuna kaburi lililofukuliwa, lakini hawakufanikiwa kupata uthibitisho.

Baada ya kushindwa kubaini mmiliki au asili ya jeneza hilo, waliwasiliana na Jeshi la Polisi, ambao walifika na kulichukua kwa uchunguzi zaidi.




No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso