Agosti 03 mwenge wa Uhuru 2025 ulikabidhiwa katika Mkoa Wa Shinyanga katika kituo cha mabasi Kagongwa Wilayani Kahama Kimkoa na kuanza ziara yake Wilayani Kahama siku hiyo hiyo, na baadae Agosti 04 kukagua miradi saba yenyethamani ya Bilioni 3.3 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu na leo Agosti 5 umekagua miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya bilioni 1. 6 katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga
Miradi iliyofikiwa na mwenge wa uhuru ni ufunguzi wa nyumba ya mtumishi katika zahanati ya ntobo, kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji kata ya Ntobo unaotekelezwa na RUWASA, makabidhiano ya pikipiki za magurudumu mawili kwa vijana wa kikundi cha Hatushindwi, kukagua ujenzi wa soko katika kituo cha mabasi Segese, kufungua shule shikizi iliyopo Segese, Na kuweka jiwe la msingi mradi wa matumizi ya nishati safi katika shule ya sekondari mwalimu nyerere.
Akipokea mwenge huo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Bi. Rose Manumba kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasauri ya Wilaya ya Ushetu Hadija Kabojela amesema miradi hiyo inahusisha miradi katika sekta ya elimu, maji, afya, mazingira, pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana na wanawake.
“Mwenge wa uhuru katika halmashauriya Wilaya ya Msalala utakimbizwa katika Kilomita 32, utafungua, utaona na utaweka mawe ya msingi katika miradi yenye thamani ya Bilioni 1 na milioni 63”
Akiwa katika mradi wa uzinduzi na makabidhiani ya Pikipiki za magurudumu mawili (boda boda) Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ali Ussi, ametoa wito kwa vijana wanaojihusisha na shughuli ya boda boda kuepuka vitendo vya uhalifu na badala yake kutumia fursa hiyo kama shughuli halali ili kujipatia kipato kwa njia za uadilifu na nidhamu.
Ussi amesema kuwa sekta ya bodaboda imeendelea kuwa mkombozi mkubwa kwa vijana, japo wengi wamekuwa wakiitumia sekta hiyo kwa ajili ya kufanikisha uhalifu wao na kusisitiza kuwa ni lazima ajira hiyo ifanywe kwa uaminifu, uwajibikaji na kuepuka kutumia pikipiki hizo kama kichaka cha uhalifu au matumizi ya dawa za kulevya.
“Mnatakiwa kuwa waaminifu, mjiwekee malengo, Kazi kama bodaboda ni ajira halali, ichukulieni kwa uzito na siyo uchochoro wa kutenda uhalifu, Amani ya nchi ni jukumu letu sote,” alisema Ussi.
Kwa upande wake, Frank Charles, Katibu wa Kikundi cha *Hatushindwi*, ameipongeza Serikali kupitia Rais Dkt. Samia kwa kurejesha mikopo hiyo muhimu kwa vijana na kusema kuwa hatua hiyo imekuwa mwanga mpya kwa vijana wengi waliokosa ajira rasmi.
“Kwanza kabisa nipende kuishukuruserikali yetu ya awamu ya Sita chini ya Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa vijana na leo tunanufaika na mkopo huu ambao utaenda kutusaidia kuendeshea maisha yetu kutokana na vipato vya kila siku” Alisema Frank
Katika upande mwingine, wananchi nao wamehimizwa kuwaunga mkono vijana hao kwa kuwatumia huduma za usafiri ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa jamii na kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa vijana.
Katika makabidhiano hayo Pikipiki hizo tano ambazo ni zao la mapato ya ndani zenye thamani ya milioni 13.5 zimekabidhiwa kwa kikundi cha vijana cha “Hatushindwi”, kilichonufaika na mkopo wa asilimia 10 kutoka halmashauri hiyo kwa malengo ya kusogeza karibu huduma ya usafirishaji na kuongeza kipato chao
Mbio hizo zinaendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi huku zikiwa na kaulimbiu mbali mbali kama vile “Shiriki uchaguzi wa 2025 kwa amani na utulivu, Afya ni mtaji zingatia unachokula, na Ziro Malaria inaanza na mimi, inaanza na wewe, inaanza na sisi sote” na msisitizo mkubwa ni katika ile inayohamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Octoba 29, 2025










No comments:
Post a Comment