
Mratibu wa TACTIC kutoka Urban Solution – Dar es Salaam, Elias Nyabusani akizungumza na waansidhi wa habari mara baada ya mkutano na wadau
NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL KAHAMA
Katika juhudi za kuupanga mji wa Kahama kwa ufanisi zaidi na kukabiliana na changamoto za ukuaji wa kasi, Mradi wa Kuboresha Miundombinu na Ushindani wa Miji ya Tanzania (TACTIC) umetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.14 kwa ajili ya maandalizi ya Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Mji huo.
Akizungumza leo Julai 4, 2025 na waandishi wa habari, mara baada ya mkutano wao na wadau, Mratibu wa TACTIC kutoka Urban Solution – Dar es Salaam, Elias Nyabusani, amesema kuwa mpango huu ni matokeo ya mchakato wa muda mrefu wa maombi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, ambayo imekuwa ikihitaji upangaji madhubuti wa mji kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.
“Kahama ni mji unaokua kwa kasi pia Kuna shughuli nyingi kama biashara, kilimo na uchimbaji madini, lakini haukupangwa ipasavyo, Ndiyo maana Mpango Kabambe unahitajika ili kuweka msingi thabiti wa maendeleo ya sasa na ya baadaye,” amesema Bw. Nyabusani.
Baada ya kukamilika na kutekelezwa, mpango huu unatarajiwa:Kupunguza migogoro ya ardhi kwa kuweka matumizi ya ardhi wazi na rasmi, Kuweka mazingira bora kwa uwekezaji kupitia miundombinu ya kisasa kama barabara, maji na huduma nyingine, Kuboresha maisha ya wakazi kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kama shule, hospitali na masoko, Kuimarisha ushindani wa mji wa Kahama kitaifa na kimataifa kwa kuwavutia wawekezaji.
Akifafanua maana ya Mpango Kabambe Mtaalamu kutoka ICE - Urban Solution Co. Ltd Hamisi Mkoma amesema ni ramani ya muda mrefu ya maendeleo ya mji, inayobainisha matumizi mbalimbali ya ardhi kama makazi, biashara, viwanda, huduma za kijamii, barabara, maeneo ya wazi, na mengineyo. Lengo kuu ni kuhakikisha miji inakua kwa mpangilio unaowezesha ustawi wa kijamii, kiuchumi na kimazingira.
Mkoma ameeleza kuwa wananchi watashirikishwa kikamilifu katika hatua zote za uandaaji wa mpango, ikiwemo mikutano ya hadhara, ukusanyaji wa maoni, na uwasilishaji wa rasimu kabla ya kuidhinishwa rasmi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Bw. Robart Kwela, amesema kuwa huu ni mradi wa kipekee ambao utabadilisha kabisa sura ya mji huo na kuuwezesha kukua kwa njia endelevu.
“Mradi huu ni wa gharama kubwa, Tunashukuru serikali kwa kutuchagua kuwa miongoni mwa halmashauri za kwanza nchini kufaidika, Zaidi ya hayo, mpango huu wa miaka miwili utafanyika kwa njia ya kidijitali,” amesema Kwela.
“Mpango huu utaziunganisha taasisi zote zinazotoa huduma – iwe ni TANESCO, TTCL au idara ya maji – ili wote wajue mji umeandaliwa vipi, hivyo kusaidia utendaji wa kazi kwa ufanisi,” ameongeza.
Aidha, amefafanua kuwa manispaa hiyo ina jumla ya mitaa 32 na vijiji 45, na matarajio ni kuwa baada ya utekelezaji wa mpango huu, maeneo yote yatapangwa rasmi kama mitaa, hivyo kuondoa mfumo wa vijiji.
Mmoja wa wadau waliohudhuria mkutano huo, Anna John kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) – Wilaya ya Kahama, amesema:“Mradi huu utasaidia sana kuondoa migogoro ya mipaka kati ya maeneo ya hifadhi ya misitu na vijiji, kwani kila upande utakuwa na uelewa wa mipaka yake.”
Manispaa ya Kahama inatarajiwa kuwa mfano bora wa upangaji wa miji kwa njia jumuishi, endelevu na rafiki kwa mazingira kwani ni Manispaa ya kwanza nchini kuingia katika mradi huo ambao utafanyika kidigitali.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Bw. Robart Kwela akizungumzia mradi kabambe wa TACTIC jinsi utakavyonufaisha wakazi wa Kahama
No comments:
Post a Comment