Afisa usimamizi wa kodi, mkoa wa kikodi Kahama Khamis Sanze akizungumza.
Na Neema Nkumbi Kahama, Shinyanga – Juni 19, 2025
Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) imeandaa jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali, likiwa na lengo la kujenga uwezo wa pamoja (capacity building), kuongeza uelewa wa taratibu za usimamizi, pamoja na kubaini mchango halisi wa mashirika haya katika maendeleo ya Taifa.
Tukio hilo muhimu limefanyika, Manispaa ya Kahama, na limekutanisha zaidi ya mashirika 40 pamoja na wadau kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Kahama, wakiwemo wawakilishi wa Serikali, taasisi za umma na mashirika ya kiraia.
Ushiriki wa Wadau na Mijadala ya Kina
Akizungumza mara baada ya kufungwa kwa jukwaa hilo, Mwenyekiti wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Shinyanga, Bakari Juma, amesema jukwaa hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwezesha mijadala ya wazi, ambapo washiriki walipata elimu juu ya taratibu za usajili, masuala ya kikodi, pamoja na namna bora ya kuendesha mashirika kwa ufanisi.
“Kumekuwa na sintofahamu kuhusu sheria za kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, lakini kupitia jukwaa hili, TRA wametoa elimu ya kutosha na kujibu maswali ya washiriki. Hili ni jambo la kupongezwa,” amesema Bakari.
Ujumbe wa Serikali kwa Mashirika
Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Bestina Gunja, ameyahimiza mashirika kufuata taratibu kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi. Ametoa wito kwa mashirika kujitambulisha rasmi kwa ofisi ya mkuu wa mkoa hasa kwa miradi yenye thamani ya kuanzia shilingi milioni 20.
“Ni lazima mashirika yafike kujitambulisha kwa ajili ya usalama na uratibu wa shughuli zao. Vilevile tunasisitiza utoaji wa taarifa za maendeleo kila robo mwaka ili serikali iweze kufuatilia matokeo ya miradi hiyo,” amesema Gunja.
Elimu Kutoka Kwa Taasisi Mbalimbali
Mashirika pia yalipatiwa elimu kutoka kwa taasisi mbalimbali zikiwemo:
TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) – Afisa Khamis Sanze amesisitiza mashirika kufuata utaratibu wa usajili, na kueleza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yasiyo na shughuli za kibiashara yanapaswa kuomba msamaha wa kodi kwa mujibu wa sheria.
NSSF (Mfuko wa Hifadhi ya Jamii) – Afisa Margareth Mwaibasa amehamasisha wananchi na wajasiriamali kujiunga na ‘Hifadhi Skimu’ ili kunufaika na mafao ya pensheni, ulemavu, uzazi, matibabu, na msaada wa mazishi.
TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) – Bi. Happiness Bilakwate alisisitiza uzingatiaji wa maadili, akitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na mashirika kubadili malengo ya awali ya uanzishaji na kutumia vibaya fursa zilizopo kwa maslahi binafsi.
Msimamo wa Serikali: Hakuna Nafasi kwa Mashirika Bubu
Katika hotuba yake, Gunja ameonya kuhusu mashirika “bubu” ambayo hayajasajiliwa ipasavyo na yanayohatarisha taswira ya mashirika mengine yanayofanya kazi kwa uadilifu.
“Tunapambana kuhakikisha mashirika haya yanafuata sheria, mila na maadili ya Mtanzania. Mashirika yatakayokwenda kinyume, Serikali haitasita kuchukua hatua stahiki,” aliongeza.
Happiness Bilakwate Afisa muelimishaji kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa wilaya ya Kahama
Afisa Maendeleo ya jamii wa Mkoa wa Shinyanga Bestina Gunje, akizungumza.
Afisa usimamizi wa kodi, mkoa wa kikodi Kahama Khamis Sanze akizungumza.
No comments:
Post a Comment